Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, mara nyingi hulazimika kuwabadili viongozi mara kwa mara ili kuepusha madhara zaidi kwa Serikali na wananchi ambayo yangeweza kutokea.
Kauli hiyo ameitoa kwenye ufunguzi wa semina elekezi kwa mawaziri, manaibu waziri,makatibu na manaibu katibu wakuu iliyofanyika leo jijini Arusha
Amesema hana lengo na hapendi kubadilisha viongozi mara kwa mara kwa kuwa anafahamu madhara yake, ikiwemo kuchukua muda mrefu kuwajenga viongozi wapya.
“Mimi sio lengo langu kubadilisha viongozi mara kwa mara, kwa kuwa huchukua muda mrefu kuwajenga. Hata hivyo, wakati mwingine nalazimika kufanya hivyo ili kuepusha madhara zaidi serikalini na kwa wananchi,” amesema Rais Samia.
Pia ameeleza kwamba wakati mwingine kufanya hivyo kuna fanya viongozi wasiwe na mipango ya muda mrefu kutokana na hofu walizonazo juu ya kutenguliwa kwa nafasi walizonazo.
“Ninafahamu madhara ya kubadilisha viongozi mara kwa mara na huwa sipendi kufanya hivyo sababu kunafanya watu wafanye kazi kwa hofu na viongozi wasiwe na mipango ya muda mrefu kwa kuhofia teuzi zao kutenguliwa. Kiongozi anapoondoshwa kazini ni fedheha kwa familia yake na watoto ambao walikuwa wanamuona mtu wa mfano.”
Akizungumzia semina hiyo elekezi, Rais Samia amesema kutokufanyika kwake mara kwa mara, kumeleta athari serikalini kwa kutengeneza ombwe la uelewa wa taratibu za utendaji kazi.
“Kutokufanyika kwa mikutano kama hii kwa muda mrefu kumeleta athari zinazoonekana wazi katika utendaji serikalini, kumekuwepo na ombwe la uelewa wa taratibu za utendaji kazi serikalini na hii ni moja ya sababu ya viongozi kubadilishwa mara kwa mara, ili kuepusha serikali na fedheha ya kuwa na viongozi wanaozifanya wizara kuwa sehemu ya malumbano na migawanyiko isiyo na tija,” amesema Rais Samia.
Aidha amewataka washiriki kuutumia mkutano wao wa faragha kujadili namna ya kuboresha uongozi bora.
“Mwalimu Nyerere alitueleza ili taifa letu liendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Watu tunao, siasa safi ipo sababu tunapotoka nje ya nchi sifa tunazopata ni kutokana na siasa safi tuliyo nayo. Suala la uongozi bora sasa haliko, tutakwenda kulijadili hapa,” amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine Rais Samia amewataka mawaziri kueleza mafanikio ya Serikali mara kwa mara, ili kudhibiti baadhi ya watu wanaofanya upotoshaji.
Amesema viongozi wa umma wamekuwa wazito kusema mafanikio hayo na kuacha watu wengine kuendelea kufanya upotoshaji.
“Nataka kuwakumbusha umuhimu wa kuisemea serikali kama moja ya mawasiliano nje ya Serikali. Katika eneo hili hatujafanya vizuri sana, tumekuwa wazito kuyasemea mafanikio mengi tunayopata na hivyo kuacha watu wengine kuendelea kufanya upotoshaji. Kuna usemi unaosema uongo ukisemwa mara nyingi huwa ukweli,”