Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kiko tayari kufanya mdahalo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, endapo Serikali itafanyia kazi madai yao juu ya upatikanaji tume huru ya uchaguzi na katiba mpya.
Msimamo huo umetolewa leo tarehe 15 Januari 2022 kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, ikiwa ni siku moja baada ya Makonda kutaka mdahalo na viongozi wa chama hicho.
“Msimamo wa chama ni kuwa, kama anataka mdahalo na sisi kama chama tupo tayari na hatujawahi kukimbia midahalo kama wao na chama chao. Hivyo basi, mdahalo unaweza kufanyika katika masuala yafuatayo ambayo tumeweka msimamo wetu wazi ili yatekelezwe na Serikali,” imesema taarifa ya Mrema.
Taarifa ya Mrema imetaja mambo hayo kuwa ni Serikali kuondoa bungeni miswada mitatu ya marekebisho ya sheria za uchaguzi ambayo Chadema inadai kuwa mibovu. Serikali ianzishe mara moja mchakato wa marekebisho ya katiba ya 1977 ili kuwezesha kuondoa mapungufu yaliyopo kwenye katiba hiyo ili kuruhusu maandalizi ya kuandikwa miswada mipya ya kuboresha mifumo ya ucvhaguzi.
“Serikali ianzishe mara moja mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Mwaka 1977 (Minimum reforms) ili kuwezesha kuondoa mapungufu yaliyopo kwenye Katiba hiyo ili kuruhusu maandalizi ya kuandikwa Kwa miswada mipya ya kuboresha mifumo ya chaguzi nchini na pia Serikali iwasilishe Bungeni muswada wa sheria ya kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi huo usimamiwe na Tume ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI” imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa
“Serikali iwasilishe Bungeni muswada wa Sheria wa kukwamua mechakato wa Katiba Mya ukiwa na mwelekeo (Road Map wa lini Nchi itapata Katiba Mpya) na pia Wadau tutaweza kukaa kwenye mdahalo ili kuishauri Serikali jinsi ya kuweza kupunguza ukali wa gharama za maisha na kuonyesha Kodi na tozo zipi zipunguzwe, anasa gani ziondolewe Serikalini na mkakati mzima wa kupunguza ukali wa gharama za maisha kwa Wananchi”.
Aidha, kupitia taarifa hiyo Mrema amesema mpango wa Chadema kufanya maandamano yasiyo na kikomo kuanzia tarehe 24 Januari mwaka huu, hadi Serikali itakapofanyia kazi madai yao, uko palepale.
“Hivyo basi katika kipindi hiki aweke mdahalo na Serikali ili waone ulazima wa kusikiliza na kuheshimu maoni ya Wananchi na Wadau mbalimbali wa chaguzi katika kuandaa mazingira bora ya kuwa na chaguzi huru na haki nchini, katika kipindi hiki Chama kinaendelea na maandalizi ya maandamano ya amani yatakayofanyika Jijini Dar es salaam tarehe 24 Januari, 2024” imesema taarifa hiyo