Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Tanzania mbioni kuzalisha madini ya Niobium - Mwanzo TV

Tanzania mbioni kuzalisha madini ya Niobium

Imeelezwa kwamba Tanzania ipo mbioni kuanza uzalishaji wa madini ya Niobium ambayo ni moja ya madini adimu yanayotumika katika mitambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya  utengenezaji wa  injini za Ndege na Roketi.

Hayo yamesemwa leo Bungeni  na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa  wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini Oran Njema kuwa ni lini uzalishaji wa madini ya Niobium na kiwanda cha uzalishaji wa Ferroniobium utaanza katika Halashauri ya Wilaya ya Mbeya. 

Dkt. Kiruswa amesema kuwa, mradi wa uchimbaji wa madini ya Niobium katika eneo la Panda Hill unamilikiwa na kampuni ya Panda Hill Tanzania Limited (PHTL) kwa ajili ya uzalishaji wa mazao yanayotokana na madini hayo ikiwemo zao la madini ya ferroniobium linalotokana na uchakataji wa madini ya Niobium.

Aidha, Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa, tayari Serikali imeanza majadiliano na kampuni ya Panda Hill kwa lengo la kusaini Mkataba wa Makubaliano utakaowezesha Serikali kupata umiliki wa hisa kwenye mradi huo ikiwa pamoja na manufaa mengine ya kiuchumi.

Akielezea kuhusu hisa za Serikali katika mradi huo, Dkt. Kiruswa ameeleza kwamba, kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, wamiliki wa Leseni za Kati na Kubwa za Uchimbaji Madini wamepewa sharti la kutoa hisa huru zisizofifishwa na zisizopungua  asilimia 16 kwa Serikali.

Dkt.Kiruswa amefafanua kuwa , utaratibu wa  ulipaji wa fidia kwa waguswa wa mradi unaendelea vizuri pindi utakapokamilika taratibu za kuanza ujenzi wa kiwanda cha uchataji wa madini ya niobium utaanza rasmi. 

Sambamba na matumizi katika nyanja ya sayansi ya teknolojia pia madini ya Niobium hutumika katika mitambo ya uchorongaji katika utafiti na uchakataji wa mafuta, gesi pamoja na utengenezaji wa magari.