Kanisa Katoliki Musoma lalaani Polisi kuwapiga mabomu BAWACHA kanisani

Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila, amelaani vikali tukio la Jeshi la Polisi kurusha mabomu ya machozi ndani ya eneo la kanisa wakati wa ibada, tukio lililotokea wakati wanachama wanawake wa Chadema  BAWACHA, walipokuwa wakitoka ibadani.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Askofu Msonganzila alisema Machi 8, siku inayoadhimishwa kimataifa kama Siku ya Wanawake Duniani, iliangukia Jumapili mwaka huu, hali iliyosababisha waumini wengi kuhudhuria ibada makanisani kama kawaida.

Kwa mujibu wa Askofu, kulikuwa na taarifa kwamba kundi la wanawake wa CHADEMA kupitia BAWACHA lilikuwa limepanga kuadhimisha siku hiyo katika Manispaa ya Musoma. Alisema kanisa lilipokea maombi ya kuruhusu kufanyika kwa mjadala au kongamano katika Viwanja vya Tumaini, mawasiliano ambayo alieleza kuwa yalikuwa ya kawaida ya kiutawala.

“Wasaidizi wangu walipokea barua na wakajibu kwamba wanaruhusiwa kufika kufanya mjadala au kongamano katika viwanja vya Tumaini,” alisema Askofu Msonganzila.

Hata hivyo, baadaye kanisa lilipokea taarifa kutoka kwa Jeshi la Polisi Manispaa ya Musoma likitaka mkutano huo usifanyike. Kwa mujibu wa Askofu, polisi walieleza kuwa hawaruhusu kufanyika kwa mikutano au maandamano ya kundi hilo.

Kutokana na taarifa hiyo, kanisa liliandika barua nyingine kwa waandaaji likieleza kuwa mkutano huo hautaweza kufanyika kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

Askofu Msonganzila alisema siku ya Jumapili ilipowadia, baadhi ya wanawake wa BAWACHA walifika kanisani bila kutambulika mara moja kuwa ni wanachama wa chama hicho, kwani hawakuingia wakiwa wamevaa mavazi ya chama. 

Baadaye, inadaiwa walivaa mavazi ya CHADEMA nje ya eneo la kanisa kabla ya kurejea na kushiriki ibada kama waumini wengine.

Alieleza kuwa kanisa lina kanuni ya kutoruhusu shughuli za kisiasa kufanyika ndani ya nyumba za ibada, lakini mara nyingine viongozi wa ibada hutumia busara na hekima katika kushughulikia hali kama hizo.

“Kiongozi wa ibada hakusema kabisa kwamba waliovaa mavazi ya CHADEMA waondoke. Baadaye walipotoka nje ndipo walianza kuzungumza na waandishi wa habari,” alisema.

Hata hivyo, Askofu alisema haijulikani ni nini hasa kilitokea wakati wanawake hao walipokuwa wakitoka kanisani, lakini muda mfupi baadaye polisi walianza kurusha mabomu ya machozi.

“Kwanini mabomu ya machozi yarushwe ndani ya eneo la kanisa la Jimbo Kuu Katoliki Musoma? Waliolengwa walikuwa kina mama wa BAWACHA, lakini walioathirika si wao tu. Kulikuwa na watoto wadogo, mabibi na wazee waliokuwa wakitoka ibada na wengine wakiingia misa ya pili,” alisema.

Askofu Msonganzila alieleza kusikitishwa na tukio hilo akisema matumizi ya nguvu katika eneo la ibada si dalili ya ukomavu wa kiutawala na yanaacha majeraha kwa jamii.

Alikumbusha pia tukio la vurugu lililotokea Oktoba 29, 2025, akisema jamii bado haijapona kutokana na majeraha ya tukio hilo na kwamba matukio ya aina hiyo yanaongeza maumivu kwa wananchi.

“Kupiga watu namna hii si dalili ya ukomavu. Bado hatujapona majeraha ya Oktoba 29, 2025, na waliojeruhiwa ni wengi. Mbaya zaidi unatumia nguvu katika eneo la ibada,” alisema.

Askofu huyo alisisitiza kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya raia havipaswi kuvumiliwa na akatahadharisha kuwa kujenga uadui kati ya vyombo vya dola na wananchi kunaweza kuleta athari kubwa kwa amani ya nchi.

“Matendo haya si ya haki. Ni unyanyasaji, na polisi hawakupaswa kuwa wakatili. Ukijenga uadui na raia unaalika maadui wengi kuingia katika nchi yako,” alionya.