Ripoti ya Tume:Mfumo wa kodi unahitaji marekebisho makubwa

Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi imewasilisha rasmi ripoti yake yenye jumla ya mapendekezo 284 ya kimkakati, yakilenga kufanya mageuzi ya kina katika mfumo wa kikodi nchini na kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa manufaa ya taifa. 

Uwasilishaji huo umefanyika Machi 18, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Samia Suluhu Hassan, ambapo tume imeainisha maeneo saba ya kipaumbele yanayohitaji maboresho, ikiwemo sera na sheria za kodi, mifumo ya kiteknolojia, utawala wa kodi, pamoja na mazingira ya uwekezaji na biashara.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya mapendekezo yote, 146 yanahusu maboresho ya sera na sheria za kikodi, 41 yanagusa mifumo ya TEHAMA, huku 30 yakihusu mifumo ya kiutawala. 

Aidha, mapendekezo 25 yanahusu urasimishaji wa shughuli za kiuchumi na upanuzi wa wigo wa walipakodi, 15 yanahusu kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, 14 yanahusu utatuzi wa migogoro ya kikodi, na 13 yanahusu muundo na usimamizi wa kodi. Tume imeeleza kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo utaongeza uwazi, ufanisi na utabiri katika mfumo wa kodi, hali itakayosaidia kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi wa muda mrefu.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Tume Ombeni Sefue alieleza kuwa mfumo wa sasa wa kodi una changamoto kubwa zinazowaumiza wananchi na kudhoofisha imani yao kwa serikali. Alibainisha kuwa uwepo wa kodi nyingi katika chanzo kimoja pamoja na ukosefu wa uratibu kati ya taasisi za ukusanyaji mapato kama Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) na mamlaka za serikali za mitaa (LGAs), unasababisha mrundikano wa tozo, ada na ushuru unaoongeza gharama za uendeshaji biashara. 

Kwa mujibu wa Sefue, hali hiyo imekuwa ikiwalazimu baadhi ya wafanyabiashara kukimbilia vitendo vya rushwa ili kuepuka usumbufu wa taratibu nyingi zisizo na uratibu.

Balozi Sefue alisisitiza kuwa wananchi wengi hawakatai kulipa kodi, bali wanahitaji mfumo ulio rahisi, wa haki na unaoeleweka. Aliongeza kuwa walipakodi wamepoteza imani na mifumo iliyopo ya utatuzi wa migogoro ya kodi kutokana na kile alichodai kuwa ukosefu wa uhuru wa kutosha kwa vyombo vinavyosimamia haki hizo. 

Aidha, alionya kuwa viwango vya kodi visivyotabirika na kuanzishwa kwa tozo mpya bila uratibu wa kimkakati vinaharibu mazingira ya biashara na kuwa kikwazo kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Katika hatua nyingine, tume imependekeza kuwepo kwa mfumo wa pamoja wa uratibu wa mamlaka zote zinazokusanya mapato ili kupunguza usumbufu kwa walipakodi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji bila kutumia nguvu au vitisho. Pia imependekeza kuundwa kwa mfumo rafiki wa kodi unaoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kwa kuzingatia usawa na haki katika ulipaji kodi pamoja na kupanua wigo wa walipakodi ili kuongeza mapato ya ndani.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Samia amesema serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote kwa lengo la kujenga mfumo wa kodi ulio imara, wa haki na unaochochea ukuaji wa uchumi. Ameeleza kuwa maboresho hayo yatahusisha pia kuimarisha sera ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), ili miradi mikubwa ya maendeleo iweze kutekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi, huku serikali ikibaki na jukumu la kusimamia huduma za msingi kama maji, umeme, elimu na miundombinu ya barabara.

Rais Samia pia amegusia changamoto ya kupungua kwa misaada kutoka kwa wahisani wa maendeleo, akibainisha kuwa hali hiyo inalazimu nchi kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. 

Amesema wakati mikopo ikiendelea kupatikana, misaada ya moja kwa moja imepungua kwa kiasi kikubwa, hivyo kuna ulazima wa kujitegemea zaidi kifedha ili kuendesha miradi ya maendeleo na kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, amewahimiza wananchi kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati, akisisitiza kuwa kodi ndiyo msingi wa utoaji wa huduma za umma. Amesema serikali haiwezi kutoa huduma bora bila kuwa na mapato ya kutosha, huku akiahidi kuwa maboresho ya mfumo wa kodi yataondoa mianya ya ukwepaji na kuhakikisha usawa katika ulipaji kodi kwa wananchi wote.