Lissu: ‘Maneno Ya Kisiasa Hayawezi Kunifanya Nipatikane Na Hatia Ya Uhaini’

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ameiambia Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa ushahidi uliotolewa katika kesi ya uhaini inayomkabili haujathibitisha kwamba maneno aliyoyasema katika mkutano wa kisiasa yanakidhi vigezo vya kosa la uhaini kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Lissu: ‘Maneno Ya Kisiasa Hayawezi Kunifanya Nipatikane Na Hatia Ya Uhaini’

Lissu amesema hayo leo Septemba 23,2026, wakati akiwasilisha hoja zake za mwisho mbele ya jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Dastun Ndunguru, akieleza kuwa tangu mwanzo wa kesi hiyo msimamo wake umekuwa kwamba hakatai kusema maneno yanayodaiwa, bali anapinga tafsiri kwamba maneno hayo yanaunda kosa la jinai la uhaini.Amesema alikamatwa mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, jioni ya Aprili 9, 2025, baada ya kuhutubia mkutano wa Chadema na kusafirishwa usiku huo hadi Dar es Salaam, ambako siku iliyofuata, Aprili 10, 2025, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili, likiwamo la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu.Kwa mujibu wa Lissu, kesi iliyofikishwa Mahakama Kuu ilitokana na shtaka la uhaini lililoanza Kisutu kabla ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuwasilisha taarifa Mahakama Kuu kuhusu tuhuma hizo Agosti 12, 2025.Katika taarifa hiyo, upande wa mashtaka unamtuhumu Lissu kuwa akiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitengeneza nia ya kuhamasisha umma na kuwezesha kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa lengo la kuitishia Serikali, na kwamba alidhihirisha nia hiyo kupitia maneno aliyoyasema na kuyachapisha.Maneno hayo ni pamoja na kauli kuhusu kuzuia uchaguzi, kuhamasisha uasi na kuvuruga uchaguzi, ambayo upande wa mashtaka umeyatumia kama msingi wa shtaka dhidi yake.Lissu amesema katika maelezo ya ziada yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka alidaiwa kuwa ndiye aliyeitisha mkutano wa watia nia wa Chadema uliofanyika Aprili 3, 2025, na kwamba ndiye aliyewaalika waandishi wa habari kutoka Mwananchi Communication Limited, Jambo TV na Clouds Media.Pia amesema upande wa mashtaka ulidai kuwa kauli zake ziliwachochea baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwamo Arusha, Kilimanjaro, Ruvuma, Dar es Salaam na Mbeya, kuhamasishana kwa lengo la kuzuia uchaguzi mkuu kwa kutumia nguvu.Katika hoja zake, Lissu amesisitiza kuwa hajawahi kukataa kusema maneno yanayodaiwa na upande wa mashtaka.

Amesema tayari aliieleza Mahakama wakati wa usikilizwaji wa awali kwamba ni kweli alitamka maneno hayo, lakini hoja yake kubwa ni iwapo maneno hayo yanaweza kisheria kuunda kosa la uhaini.Ameongeza kuwa maneno hayo hayakusemwa mara moja katika mkutano mmoja pekee, bali aliyasema katika maeneo mbalimbali likiwamo Njombe, Lindi, Mbeya na Mtwara.Kwa msingi huo, Lissu amesema utetezi wake haujawahi kuwa wa kukana kauli hizo, bali umekuwa ukijikita katika hoja kwamba maneno hayo si uhaini wala kosa jingine la jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania.Lissu pia ameieleza Mahakama kuwa kesi yake ni miongoni mwa kesi za uhaini zilizowahi kufunguliwa Tanzania chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu.Amesema kesi mbili zilizotangulia, zilizowahusu Grey Likukungu na wenzake mwaka 1970 pamoja na Khatibu Ghandi na wenzake mwaka 1983, zilihusisha tuhuma za kuipindua Serikali, tofauti na kesi yake ambayo, kwa mujibu wake, inahusu tuhuma za kuitishia Serikali.Kwa sababu hiyo, amesema uamuzi wa Mahakama katika kesi yake unaweza kuweka msingi wa kisheria kuhusu tafsiri ya kosa la uhaini linalodaiwa kufanywa kwa kuitishia Serikali.Katika hoja zake, Lissu ameitaka Mahakama iamue iwapo ndiye aliyeitisha mkutano wa Aprili 3, 2025 na kama ndiye aliyewaalika waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo.Pia ameomba Mahakama iamue iwapo maneno anayodaiwa kuyasema yanaunda kosa lolote la jinai na, kama yanafanya hivyo, iwapo kosa hilo ni uhaini.Masuala mengine aliyoyaibua ni iwapo maneno yanaweza kuchukuliwa kuwa matendo, iwapo alichapisha maneno hayo kupitia YouTube ya Jambo TV, na iwapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitishika kutokana na maneno hayo.Mwisho, amehoji iwapo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi yake kwa kiwango kinachotakiwa na sheria na aina ya hukumu ambayo Mahakama inapaswa kutoa kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa.Lissu amewataka majaji kuzingatia kanuni mbalimbali za sheria za jinai, ikiwamo kwamba sheria zinazoweka adhabu zinapaswa kutafsiriwa kwa umakini mkubwa na kwamba mzigo wa kuthibitisha mashtaka unabaki kwa upande wa mashtaka.Amesema pia ushahidi unapaswa kupimwa kwa ujumla wake na si kwa kuangalia vipande vya ushahidi mmoja mmoja, huku akisisitiza kuwa hatia inapaswa kutokana na nguvu ya ushahidi wa mashtaka badala ya udhaifu wa utetezi.Katika hoja zake kuhusu uhaini, Lissu ameitaja pia misingi inayohusu maana ya “kuchapisha”, hitaji la kuthibitisha kitendo cha wazi katika kesi ya uhaini pamoja na hoja kwamba maneno matupu hayawezi kuunda kitendo cha wazi cha uhaini isipokuwa pale maneno hayo yanapoelezea matendo.Akianza kuchambua ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Lissu ameanza na tuhuma kwamba ndiye aliyeitisha mkutano wa watia nia wa Chadema uliofanyika Aprili 3, 2025.Amesema kati ya mashahidi 17 wa upande wa mashtaka hakuna aliyetoa ushahidi unaoonyesha namna mkutano huo ulivyoitishwa wala kumtaja yeye kuwa ndiye aliyeitisha mkutano huo.Pia amesema upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa nyaraka kuthibitisha tuhuma hiyo.Kwa upande mwingine, amesema ushahidi wa utetezi, ukiwamo wa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, unaeleza kuwa mkutano huo uliitishwa na kuandaliwa na Sekretarieti ya Chadema baada ya Mnyika kuelekeza kufanyika kwake.Lissu amesema ushahidi huo uliungwa mkono na mashahidi wengine wa utetezi, akiwamo Amani Golugwa na Brenda Rupia, hivyo kwa mtazamo wake tuhuma kwamba ndiye aliyeandaa mkutano huo haijathibitishwa.Kuhusu tuhuma kwamba yeye ndiye aliyewaalika waandishi wa habari kwenye mkutano huo, Lissu ameieleza Mahakama kuwa tuhuma hiyo si ya kweli.Amesema katika maelezo ya ziada yaliyowasilishwa wakati wa usikilizwaji wa awali, upande wa mashtaka ulisema waandishi wa habari walialikwa kwenye mkutano huo, lakini haukueleza ni nani aliyewaweka mwaliko.Kwa mujibu wa Lissu, baadaye mashahidi wa mashtaka walitoa ushahidi ukidai kuwa yeye ndiye aliyewaalika waandishi hao kwenye mkutano huo.Ametaja ushahidi wa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Kamishna Msaidizi wa Polisi George Bagemu, aliyedai kuwa Lissu aliwaalika waandishi ili hotuba yake iweze kusikilizwa na watu wote, huku akisema ushahidi huo uliungwa mkono na shahidi wa pili, Inspekta John Kahaya.Kesi inaendelea