Chama cha ODM kinatarajiwa kuandaa zoezi la kitaifa la kuwasha mwanga wa mishumaa Ijumaa, Oktoba 2, 2026 kumukumbuka aliyekuwa kiongozi wao na Waziri Mkuu wa Kenya marehemu Raila Odinga, mwaka mmoja baada ya kifo chake.
Zoezi hilo litafanyika kwa wakati mmoja katika kaunti zote 47 kuanzia saa kumi na mbili jioni, huku Wakenya wakihimizwa kuwasha mishumaa walipo wakiwemo walioko katika makao makuu ya kaunti na maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
ODM imeweka wazi kuwa zoezi hilo limeandaliwa kwa ushirikiano na Kamati ya kitaifa inayosimamia maandalizi ya kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa kifo cha Odinga. Tangazo hilo lilifuata mawasiliano ya chama baada ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Septemba 9, 2026.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa ODM ambaye ndiye Gavana wa Jimbo la Homa Bay Gladys Nyasuna Wanga, wakenya nchini na wale walioko Ughaibuni wanahimizwa kushiriki katika zoezi hilo la kiongozi aliyetajwa kama Baba wa ugatuzi na demokrasia nchini Kenya.
Wanga amesema taifa lilimpoteza kiongozi mashuhuri mwaka mmoja uliopita, akisisitiza kuwa urithi na kumbukumbu za marehemu Raila zinaendelea kuishi miongoni mwa wakenya daima dawamu.
Katika Jiji kuu la Nairobi, shughuli kuu itafanyika katika uwanja wa Uhuru Park kuanzia saa tisa alasiri, huku zoezi la kuwasha mishumaa likitarajiwa kuanza rasmi saa kumi na mbili jioni. Viongozi wa kitaifa wa chama hicho wanatarajiwa kuwaongoza wafuasi kindakindaki wa chama na wakenya kwa ujumla katika uwanja huo.
Katika kaunti ya Mombasa washirika watakongamana katika eneo la Treasury Square huku Kisumu shughuli hiyo ikifanyika eneo la Kisumu Central Square.
Uongozi wa ODM umesema shughuli za mwezi wa Oktoba zinalenga kuwapa wakenya nafasi ya kumkumbuka kiongozi wao Raila Odinga, kutafakari kuhusu maadili aliyosimamia, masuala aliyopigania pamoja na mchango wake katika jamii ya Kenya. Chama hicho kimetaja Oktoba kuwa “Mwezi wa Baba” huku kikiwahimiza wakenya kutoka maeneo mbalimbali kuwasha mishumaa kwa ajili ya Baba Raila Odinga.
Raila Odinga aliaga dunia Oktoba 15, 2025, akiwa na umri wa miaka 80 wakati akipokea matibabu nchini India. Kifo chake kilifuatwa na maombolezo ya kitaifa na mazishi ya yaliyofanyika katika makaazi rasmi ya familia yake eneo la Kang’o Ka Jaramogi eneo la Bondo kaunti ya Siaya.
Zoezi la Oktoba 2 litakuwa mwanzo wa shughuli za mwezi mzima zilizoandaliwa na ODM kuelekea maadhimisho yam waka mmoja wa kifo cha Raila, ambayo kilele chake kitakuwa Oktoba 15.







