Rais William Ruto ameeleza kwa mara ya kwanza sababu zilizopelekea Kaunti ya Lamu nchini Kenya ikachaguliwa kama eneo bora zaidi kujengwa kiwanda cha kusafisha mafuta, akisema uamuzi huo ulitokana na tafiti za kitaalamu zilizoonyesha kuwa eneo hilo linafaa zaidi kwa kushughulikia mafuta ghafi.
Rais Ruto akizungumza katika Ikulu ya Mombasa, alisema serikali yake hapo awali ilikuwa imezingatia maeneo mbalimbali, yakiwemo Tanga nchini Tanzania katika kusaka eneo linalofaa kwa ujenzi wa kiwanda hicho cha kusafisha mafuta ambacho kingehudumia Kenya na eneo la Afrika Mashariki.
Kauli ya Rais Ruto inajiri siku moja tu baada ya Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni kuunga mkono mradi huo ila akaweka wazi kuwa Uganda haitawekeza katika mradi huo hadi pale itakapobaini kilichopelekea mradi huo kutojenga Tanga Tanzania jinsi ilivyokuwa umepangwa.
Rais Ruto hata hivyo, amesema mjadala huo ulihusishwa na mipango ya awali ya kujenga bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Pwani ya Kenya.
Kwa mujibu wa Rais Ruto, Uganda wakati huo ilikuwa ikizingatia kusafirisha mafuta yake kutoka maeneo ya Hoima hadi Mombasa ila baada ya kutokuwepo kwa mwafaka kati ya Kenya na Uganda, mradi wa bomba ulielekezwa kupitia Tanzania hadi Tanga.
Mabadiliko hayo yalifanya Tanga kuzingatiwa kama eneo linaloweza kujengwa kiwanda cha kusafisha mafuta kwa ajili ya eneo la Afrika Mashariki.
“Tulifikiri huenda kingejengwa Tanga kwa sababu hapo ndipo mafuta ghafi kutoka Uganda yalitarajiwa kuelekeza,” amesema Rais Ruto.
Amesema tafiti zaidi zilizofanywa na wataalamu pamoja na maafisa wa serikali zilibaini kuwa kaunti ya Lamu ilikuwa na mazingira bora kwa mradi huo.
Rais Ruto ameeleza kuwa moja ya wasabu kuu ilikuwa kina cha maji ya bahari ya Lamu, ambacho kingewezesha meli kubwa zinazobeba mafuta ghafi kufika katika eneo hilo.
“Utafiti zaidi ulifanywa, ukihushisha wawekezaji na maafisa wetu na hatimaye ikaafikiwa kuwa kiwanda kijengwe Lamu na wala si Tanga,” alisema.
Amesisitiza kuwa Lamu pia lina umuhimu wa kimkakati katika kushughulikia bidhaa za mafuta na kukuza shughuli za viwanda katika eneo la Pwani.
Kulingana na Rais Ruto, mradi huo hautalenga tu kusafisha mafuta ghafi bali pia utatoa fursa za uzalishaji wa umeme, biashara, uwekezaji na uanishwaji wa viwanda vinavyotumia bidhaa za mafuta kama malighafi.
Rais aidha, amesema kiwanda hicho kinaweza kuchochea ukuaji wa viwanda vya kutengeneza plastiki na bidhaa za petrochemical, pamoja na biashara nyingine zitakazohitaji bidhaa zitakazozalishwa katika kiwanda hicho.
Rais Ruto ameshikilia kuwa mjadala kuhusu ujenzi wa kiwanda hicho umekuwa ukiendelea kwa miaka kadhaa huku serikali ikilenga kuanzisha kituo kitakachohudumia Kenya pamoja na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Alikumbuka pia kukutana na mfanyibiashara bwenyenye wa Nigeria Aliko Dangote, katika mkutano uliokuwa Jijini Nairobi ambapo alisema mfanyibiashara huyo alihimizwa kuzingatia kuwekezaji katika mradi huo.
Ruto amesema Dangote baadaye alitembela Kenya na mazungumzo kuhusu kiwanda hicho pamoja na uwekezaji mwingine yakaendelea.
Alisema mradi huo uliendelezwa kma sehemu ya mipango ya kuifanya Lamu kuwa kitovu cha viwanda na usafirishaji wa bidhaa.
Kwa mujibu wa Ruto, eneo hilo lina miundombinu na mazingira ya baharini yanyohitajika kwa mradi mkubwa wa mafuta huku likiwa na nafasi ya kutosha kwa viwanda vingine vinavyohusiana na mradi huo kuanzishwa.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa sehemu kubwa la viwanda litakalojumuisha shughuli za mafuta, utengenzaji wa plastiki na viwanda vingine vinavyotumia bidhaa za mafuta kama malighafi.
Rais Ruto amesisitiza kuwa uamuzi wa serikali kuchagua Lamu ulizingatia tathmini za kitaalamu pamoja na uwezo wa eneo hilo kuchochea mfumo mpana wa viwanda, badala ya kuangalia ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta pekee.








