Sifuna: Maisha Yangu Yamebadilika Pakubwa Mwaka Mmoja Uliopita

Victor Wanaswa Avatar

Nyota ya kisiasa ya Seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Watenya Sifuna imeonekana kung’aa kwa kiwango kikubwa baada ya kufariki kwa aliyekuwa Kinara wa upinzani wa muda mrefu nchini Kenya hayati Raila Odinga.

Migawanyiko ya kisiasa iliyosababishwa na urithi wa uongozi wa chama cha ODM kufuatia kifo cha Odinga, kilipelekea Sifuna kuibuka kisiasa na hata kuelezewa na wengi kama kimbuka kikali kinachochipuka ambacho hakiwezi kupuuzwa.

Hata hivyo Sifuna mwenyewe anasema maisha yake yamebadilika pakubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, huku akisimama kidete kuwa Safari yake ya kuelekea Ikulu katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027 Iiko imara.

Akizungumza katika Seneti wakati wa mjadala kuhusu uteuzi wa Kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC), Sifuna alisema kuwa safari yake ya kisiasa katika kipindi cha miezi 12 iliyopita imekumbwa na misukosuko ila akatoa hakikisho kuwa hajayumbishwa katika azma yake ya kutaka kumbandua Rais Ruto uongozini katika uchaguzi mkuu mwakani.

Seneta huyo ambaye alihudumu kama katibu mkuu wa chama cha ODM chini ya Hayati Raila Odinga kwa takriban miaka minane, anasema awali angeweza kuzuru maeneo mbalimbali ya Jiji Kuu la Nairobi na hata maeneo mengine nchini ila hali hiyo sasa imebadilika kutokana na mazingira yake ya kisiasa.

“Maisha yangu yamebadilika sana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Harakati zangu zimewekewa vikwazo sana, niko chini ya uangalizi wa mamlaka saa 24 na watu wengi katika maeneo niliyokuwa nikitembelea hawajaniona kwa zaidi ya miezi 12,” alisema Sifuna.

Sifuna hata hivyo, alisema anaamini kuwa hali hiyo itabadilika baada ya uchaguzi mkuu ujao. Amesisitiza kuwa mabadiliko ya kisiasa yanaweza kumfanya kiongozi aliyekuwa upande wa upinzani kuingia serikalini na kurejelea uwezekano wa yeye mwenyewe kuwa katika Serikali ijayo.

Ikumbukwe kuwa mikutano ya kundi la Linda Mwananchi imekuwa ikivurugwa na wahuni wa kisiasa, kilele kikiwa Agosti 17 mwaka huu ambapo mtu mmoja alipoteza Maisha yake huku wengine 46 wakijeruhiwa katika mkutano wao kaunti ya Homa Bay.

Sifuna pia alizuiliwa kuingia katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolijia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) wiki mbili zilizopita baada ya uongozi wa Chuo hicho kupinga Kongamano la Wanafunzi alikokuwa amealikwa kuhutubia.

Masaibu ya kiongozi huyo yalianza alipofautiana na baadhi ya viongozi wa chama cha ODM kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya mpango wa Serikali Jumuishi ulioundwa kati ya serikali ya Kenya Kwanza na baadhi ya viongozi wa upinzani.

Kutokana na msimamo huo, Sifuna alivuliwa kama Katibu Mkuu wa ODM na kuondolewa katika baadhi ya nafasi za uongozi wa Bunge la Seneti, hatua iliyochangia kuongezeka kwa mvutano wake wa kisiasa na uongozi wa ODM.

Hata hivyo, Sifuna ameshikilia kuwa serikali ambayo Muungano wa upinzani utaunda itatimiza ahadi zote ilizowapa wakenya.

“Tunakusudia kutimiza kila ahdi tuliyowapa wananchi wa Kenya, ikiwemo ahadi ambayo nimeitoa hivi karibuni,” alisema Kiongozi huyo.

Msimamo wa Sifuna umeendelea kuvutia uangalizi wa kisiasa huku akijipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, ambako amehusishwa na mpango wa Linda Mwananchi.

Katika hatua nyingine iliyotajwa kama afueni kwa kundi hilo, Mahakama ya Migogoro ya Vyama vya Kisiasa nchini (PPDT) ilitengua uamuzi wa msajili wa Vyama vya Kisiasa wa kukataa kuhifadhi jina la Linda Mwananchi.

Jopo hilo liliamuru Msajili wa Vyama vya Kisiasa kuhifadhi jina hilo ndani ya siku saba, ikisema uamuzi wa awali wa kulikataa haukuwa na msingi wowote wa kisheria.

Jopo hilo lilisema Liberty National Democratic Alliance maarufu kama LINDA, haikuwa chama cha kisiasa kilichosajiliwa kikamilifu na hivyo hakikuwa na uwezo wa kisheria kushiriki katika kesi hiyo kwa jina lake.

Uamuzi huo umeondoa kikwazo cha kisheria kilichokuwa kimeikabili Linda Mwananchi, huku Sifuna na wandani wake wakiendelea na maandalizi ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.

 

 

 

Our Correspondent Avatar