Mahakama Kuu ya Mombasa imewapata mhubiri mwenye utata Paul Nthenge Mackenzie na washtakiwa wenzake 28 na hatia ya vifo vya watu 191 katika mkasa wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.
Katika uamuzi uliotolewa Jumatatu, Oktoba 19, 2026, mahakama iliwapata na hatia ya kuwapotosha na kuwafanya wafuasi wao kuwa na misimamo mikali ya kidini, hali iliyochangia vifo vya watoto 190 na mtu mzima mmoja.
Mahakama imepanga kutoa hukumu dhidi ya Mackenzie na wenzake Novemba 6, 2026, baada ya kesi hiyo iliyovuta hisia za umma kwa zaidi ya miaka mitatu.
Mackenzie na wenzake walikuwa wamekana mashtaka 191 ya mauaji walipofikishwa mahakamani mwaka 2024.
Wakati wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa mashahidi zaidi ya 120 kuhusu matukio yaliyotokea kati ya mwaka 2021 na 2023 katika shamba lenye ukubwa wa ekari 800 katika Msitu wa Shakahola.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa Mackenzie aliwaelekeza wafuasi wake kufunga kula, akiwashawishi kwamba kujinyima chakula hadi kufa kungewasaidia kukutana na Yesu.
Waendesha mashtaka walieleza kuwa kulikuwa na mfumo uliopangwa wa kusababisha vifo, ambapo watoto walilengwa kwanza, wakifuatiwa na vijana, wanawake na hatimaye wanaume.
Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga ushahidi wa upande wa mashtaka, wakisema kesi hiyo ilitegemea kwa kiasi kikubwa ushahidi wa kimazingira, taarifa za kusikia kutoka kwa wengine na matokeo ya uchunguzi wa kitaalamu ambayo hawakuyachukulia kuwa ya mwisho.
Mkasa wa Shakahola ulifichuka Aprili 2023 baada ya shirika la kutetea haki za binadamu kuarifu mamlaka kuhusu hali iliyokuwa ikiendelea katika eneo hilo. Operesheni ya maafisa wa polisi iliyofuata iliwawezesha baadhi ya wafuasi kuokolewa na makaburi ya halaiki kugunduliwa.
Zoezi la kuchimbua makaburi lilifichua mamia ya miili, huku idadi ya waliofariki ikiongezeka kiasi cha kulazimisha zoezi hilo kusimamishwa kwa muda baada ya vyumba vya maiti eneo hilo kukosa nafasi ya kuhifadhi miili.
Mwaka 2024, Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya iliweka idadi ya waliofariki katika mkasa huo kuwa 429, ingawa miili mingine imeendelea kuripotiwa kupatikana katika maeneo jirani. Baadhi ya waathiriwa bado hawajatambuliwa.
Mackenzie, aliyeanzisha kanisa la Good News International mwaka 2003, alikuwa amepata wafuasi kupitia matawi ya kanisa hilo jijini Nairobi na katika Pwani ya Kenya kabla ya kutangaza kulifunga mwaka 2019.
Hata hivyo, mhubiri huyo alikuwa amewahi kukumbana na mkono wa sheria. Mwaka 2017, alikamatwa kuhusiana na madai ya kueneza misimamo mikali ya kidini, lakini baadaye akaachiliwa huru katika kesi hiyo. Mwaka 2019, alikamatwa tena kufuatia vifo vya watoto wawili vilivyohusishwa na njaa huko Shakahola.
Mnamo Januari 2026, Mackenzie alikabiliwa na mashtaka mapya yanayohusiana na kupatikana kwa miili mingine 52 katika kijiji kilicho karibu na eneo la Shakahola, na kuongeza idadi ya kesi za jinai zinazomkabili kutokana na mkasa huo.
Mackenzie na washtakiwa wenzake 28 wanatarajiwa kurejea mahakamani Novemba 6, 2026, kusikiliza hukumu yao katika kesi hiyo iliyozua mjadala mkali kuhusu itikadi kali za kidini, ulinzi wa watoto na usimamizi wa taasisi za kidini nchini Kenya.








