, , , ,

Tanzania: Tundu Lissu kuanza mgomo wa kula leo?

Victor Wanaswa Avatar

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, anatarajiwa kuanza mgomo wa kula kuanzia leo, Jumatatu, Oktoba 26, 2026, akipinga kile kinachoelezwa na mawakili wake kuwa ni kushindwa kwa uongozi wa Gereza la Ukonga kutekeleza amri ya Mahakama Kuu kuhusu haki yake ya kukutana na mawakili wake kwa faragha.

Taarifa kuhusu mpango huo ilitolewa Oktoba 24 na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dkt. Nshala, uamuzi wa Lissu unatokana na kutoridhishwa kwake na utaratibu unaotumiwa na uongozi wa gereza hilo wakati anapokutana na mawakili wake, akidai kuwa hauzingatii maelekezo yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Oktoba 16, 2026, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi kuhusu haki ya Lissu kukutana na kuzungumza na mawakili wake kwa faragha. Mahakama ilielekeza kuwa maafisa wa gereza wanaweza kufuatilia mikutano hiyo kwa kumwangalia mfungwa, lakini hawapaswi kusikia mazungumzo yake na mawakili.

Dkt. Nshala alisema mawakili wa Lissu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, walipokwenda Gereza la Ukonga kumtembelea mteja wao, waliambiwa kuwa mazungumzo hayo yangefanyika huku maafisa wa gereza wakiwa ndani ya chumba hicho.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Lissu alikataa kuzungumza na mawakili wake kwa utaratibu huo, akisisitiza kuwa anataka maelekezo ya Mahakama yafuatwe.

Dkt. Nshala alisema alikwenda pia gerezani Ijumaa, Oktoba 23, kwa lengo la kukutana na Lissu, lakini alikumbana na changamoto kabla ya hatimaye kupata nafasi ya kuzungumza naye.

Alisema Lissu alimweleza msimamo wake wa kutokula chakula hadi pale haki yake ya kukutana na mawakili wake kwa faragha itakapoheshimiwa. Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Lissu pia alionyesha utayari wa kuacha kutumia dawa anazopewa, licha ya kuonywa kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kwa afya yake.

Mgomo huo unatarajiwa kufanyika wakati Lissu akiendelea kushikiliwa gerezani akikabiliwa na kesi ya uhaini, ambayo hukumu yake inatarajiwa kutolewa Novemba 6, 2026.

Our Correspondent Avatar