, , ,

Ruto amrushia Gachagua makombora, adai anawatapeli baadhi ya wagombea wa DCP

Victor Kayanda Avatar

Rais William Ruto amemshambulia vikali aliyekuwa Naibu wake Rais Rigathi Gachagua, akimtuhumu kwa kuwatapeli kifedha wanasiasa wanaotaka kuwania nyadhifa za kisiasa kupitia chama chake cha DCP, kwa kuwalazimisha kulipa mamilioni ya pesa ili kupata tiketi za chama hicho.

Akizungumza Jumatatu wakati wa ziara yake eneo la Gusii, Ruto alimtaja Gachagua kama kinara wa ulaghai wa kifedha nchini, akidai kuwa wagombeaji wanalazimishwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha ili kupata nafasi za kisiasa ndani ya chama hicho.

“Bwana Texas, wewe ndiwe kinara wa ulaghai nchini. Ulifutwa kazi kwa sababu ya unyang’anyi. Umekuwa ukiwasumbua wafanyabiashara kwa kuwaibia kupitia vitisho na madai ya fedha. Umekuwa ukiwasumbua wagombeaji wa chama chako kwa njia hiyo hiyo. Kila mtu anayekujia lazima atoe pesa. Sijui, gavana mmoja analipa milioni 10, mwingine milioni 20. Sijui wagombeaji wengine wanalipa kiasi gani. Hadi kufikia hatua ya kushika tu kipaza sauti kama hiki, ni lazima ulipe shilingi elfu 50,” Ruto alidai.

Gachagua sasa ameibukia kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa kisiasa wa Ruto, huku akiendeleza kampeni kali za kupinga kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Hata hivyo, Rais amepuuzilia mbali madai ya aliyekuwa naibu wake kwamba alichangia pakubwa kumwezesha kushinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Ruto alisisitiza kuwa alizunguka maeneo mbalimbali nchini kuomba kura, akisema ushindi wake wa urais haukuwa hisani kutoka kwa aliyekuwa naibu wake.

“Halafu anaenda kila mahali akisema, ‘Mimi ndiye niliyemfanya Ruto kuwa Rais.’ Ningependa kuwauliza nyinyi wenyeji wa Kisii, hamkunipokea niliposimama hapa kuwaomba kura?” Ruto aliuliza.

“Haukunifanya kuwa Rais. Nilizunguka nchi nzima nikiwaomba Wakenya wanichague. Wewe ni mbunge wa muhula mmoja tu, ilhali mimi nimechaguliwa mara saba,” alisema.

Aidha, Ruto alimkosoa Gachagua kuhusu matamshi yake kuhusiana na wananchi wanaohudhuria mikutano ya kisiasa ya serikali, akisema ni kuwadharau Wakenya kwa kusema wanalipwa ili kuhudhuria mikutano hiyo.

Rais alisisitiza kuwa wananchi wana uwezo wa kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu viongozi wanaowataka na hawapaswi kuchukuliwa kana kwamba wanasiasa ndio wanaowaamulia namna ya kutumia haki yao ya kisiasa.

“Hawa wananchi ni watu wako na akili. Wao ndio wataamua nani kiongozi, nani si kiongozi,” alisema Ruto.

Makabiliano haya ya hivi punde yanaashiria kuongezeka kwa ushindani kati ya viongozi hao wawili kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027.

Awali, Gachagua, ambaye anaongoza chama cha DCP, alikuwa amemtuhumu Ruto kwa kutumia fedha, vitisho na vitendo vya kuwashinikiza na kuwatisha wanasiasa wa chama chake wanaotaka kuwania nyadhifa za kisiasa.

Viongozi hao wawili walihudumu pamoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022, kabla ya uhusiano wao kuzorota na hatimaye Gachagua kujiunga na kambi ya upinzani, ambako sasa ni miongoni mwa viongozi wanaolenga kumng’oa Ruto mamlakani katika uchaguzi wa mwaka 2027.

 

Our Correspondent Avatar