Mjane wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, mama Ida Odinga, ametangaza hadharani kwa mara ya kwanza kuwa yeye bado ni mwanachama na atasalia katika chama cha ODM na ataunga mkono serikali jumuishi inayoongozwa na Rais William Ruto.
Akizungumza katika Kaunti ya Homa Bay, mama Ida alisema marehemu mumewe, Raila Odinga, alimwacha ndani ya chama cha ODM na serikali jumuishi, na kwamba hana nia ya kubadilisha msimamo huo.
Ida alisema kifo cha ghafla cha Raila kiliwaacha wengi, hususan wafuasi na washirika wake wa kisiasa, wakiwa wamechanganyikiwa kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa kufuata.
Hata hivyo, aliwataka kuendeleza misimamo ambayo marehemu Raila alikuwa amewaachia badala ya kubadili misimamo yao.
Mama Ida alizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usimamizi wa Milima ya Gembe katika eneo bunge la Suba North, akiwa ameandamana na Mbunge wa eneo hilo Millie Mabona.
“Baba alipoondoka, Mheshimiwa Raila Amollo Odinga, ambaye alikuwa mume wangu, alituacha ghafla. Baadhi ya watu walifika alipokuwa, huku wengine hawakufanikiwa kufika.
Mahali alikoniacha ndipo ninaposimama hadi sasa.”
Ida aliongeza kuwa Raila aliwaacha watu wengi, lakini kila mmoja anapaswa kuendelea kusimama katika nafasi aliyokuwa ameachwa nayo.
“Kwangu mimi, aliniacha ndani ya ODM. Ndiyo maana bado nipo hapo. Aliniacha katika serikali jumuishi, na hapo ndipo ninaposimama,” alisema Ida.
Alifichua kuwa Raila alikuwa amemweleza kuwa Rais William Ruto ndiye kiongozi wa nchi, na kwamba huo ndio ulikuwa mwelekeo aliopaswa kufuata.
Tamko hilo limeonekana kuwa pigo kwa mrengo wa Linda Mwananchi, unaojumuisha baadhi ya wanachama wa ODM wanaopinga ushirikiano wa chama hicho na serikali ya Rais Ruto, wakiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Gavana wa Siaya James Orengo, miongoni mwa wengine.
Baadhi ya viongozi hao wameunda au kujiunga na vyama vingine vya kisiasa wanavyonuia kutumia kuendeleza safari yao ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Sifuna, ambaye anaongoza chama cha Linda Mwananchi, anaendelea kuweka mikakati ya kukiunganisha chama hicho na vuguvugu la Linda Mwananchi. Muungano huo unalenga kuunganisha vyama kadhaa vinavyopinga uongozi wa Rais William Ruto ili kubuni upinzani ulio na nguvu na msimamo mmoja.
Ida aliteuliwa na Rais Ruto mwaka 2026 kuwa mwakilishi wa kudumu wa Kenya katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), nafasi ambayo bado anashikilia.
Uteuzi huo ulifanyika katika juhudi za Rais Ruto kuvutia wafuasi na ngome za kisiasa zilizokuwa zikimuunga mkono Raila Odinga kufuatia kifo chake mnamo Oktoba 15, 2025.
Familia ya Odinga inaendelea kutambuliwa kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya.







