, , ,

Ruto atetea rekodi ya utawala wake kwenye hotuba yake ya nne kabla ya uchaguzi mkuu

Victor Kayanda Avatar

Rais William Ruto ametetea rekodi yake ya katika usimamizi wa uchumi, akitaja kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Kenya, kupungua kwa mfumuko wa bei, kushuka kwa viwango vya riba za mikopo katika benki za biashara na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kama ishara kuwa nchi imevuka changamoto za kiuchumi ilizokumbana nazo mwaka 2022.

Akizungumza wakati akitoa hotuba yake ya nne kwa bunge kuhusu hali ya taifa, Ruto alisema serikali yake imechukua hatua ngumu lakini muhimu za mageuzi ya kiuchumi ili kurejesha uthabiti wa uchumi, licha ya kutokuwa na uhakika katika uchumi wa dunia na changamoto katika biashara ya kimataifa.

“Thamani ya shilingi ya Kenya imeimarika kutoka takribani shilingi 162 dhidi ya dola moja ya Marekani hadi takribani shilingi 129.” Alieleza Rais Ruto.

Kwenye hotuba hiyo iliyosheheni kauli mbiu ya Usawa ni Sawa, Ruto amesisitiza kuwa hatua hiyo ni ufanisi wenye umuhimu katika kurejesha imani ya wawekezaji na wananchi katika uchumi wa nchi.

Rais pia alibainisha kuwa viwango vya riba za mikopo katika benki za biashara vimepungua kutoka asilimia 17.2 mwezi Novemba 2024 hadi takribani asilimia 14.4 mwezi Septemba mwaka huu.

Alisema kupungua kwa gharama ya mikopo kutarahisisha upatikanaji wa fedha kwa wafanyabiashara, kuwawezesha kupanua shughuli zao na hivyo kubuni nafasi zaidi za ajira.

“Nchi yetu inarejea katika hali nzuri ya ukuaji kwa kasi. Uchumi wetu unaimarika, miundombinu inapanuliwa, mfumo wetu wa elimu unafanyiwa mageuzi na fursa mpya zinafunguliwa kwa vijana wetu kupata ajira, kujipatia kipato na kufanikiwa kimaisha,” alisema.

Aidha, Ruto alisema mfumuko wa bei, ambao ulifikia asilimia 9.6 mwaka 2022, ulipungua hadi asilimia 4.1 mwaka 2025. Hata hivyo, shinikizo jipya la kupanda kwa bei ya vyakula na nishati limesababisha ongezeko la mfumuko huo mwezi Oktoba mwaka huu.

Takwimu za hivi punde za Shirika la Kitaifa la Takwimu nchini Kenya (KNBS) zinaonyesha kuwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulipanda hadi asilimia 7.3 mwezi Oktoba 2026, kutoka asilimia 6.8 mwezi Septemba, hali iliyochangiwa zaidi na kupanda kwa gharama za vyakula, usafiri na makazi.

Rais alikiri kuwepo kwa shinikizo hilo jipya la kiuchumi, lakini akasisitiza kuwa uthabiti wa uchumi ambao serikali yake imefanikiwa kuimarisha unaiweka nchi katika nafasi nzuri zaidi ya kukabiliana na changamoto hizo.

Vilevile, alizungumzia ongezeko la akiba ya fedha za kigeni, akisema imeongezeka kutoka dola bilioni 7.3 mwaka 2022 na kufikia kiwango cha juu cha dola bilioni 15.3 mwaka huu.

Ruto alitaja ulipaji wa deni la Eurobond lenye thamani ya dola bilioni 2 lililostahili kulipwa mwezi Juni 2024 kama ushahidi mwingine wa uwezo wa nchi kutimiza wajibu wake wa kulipa madeni ya nje.

Alisema serikali ililipa deni hilo ili kulinda hadhi ya Kenya katika masoko ya kimataifa ya fedha na kurejesha imani katika uchumi wa nchi.

Rais alisisitiza kuwa mafanikio hayo hayafai kupimwa kwa kuangalia takwimu za kiuchumi pekee, bali pia namna yanavyowanufaisha wananchi na wafanyabiashara katika maisha yao ya kila siku.

Alisema sarafu imara, mfumuko wa bei unaodhibitiwa na mikopo nafuu vinawawezesha wafanyabiashara kupanga shughuli zao, wakulima kuongeza uzalishaji, wawekezaji kuunda nafasi za ajira na familia kulinda uwezo wao wa kununua bidhaa na huduma.

Rais Ruto pia ametangaza kuwa serikali yake imetoa shilingi bilioni 15.07 kwa wakulima 680,000 wa kahawa, huku pia ikitenga shilingi bilioni 1.2 kama bonasi kwa wakulima wa miwa, katika juhudi za kufufua sekta ya kilimo nchini.

Ruto alisema bei ya kilo moja ya kahawa iliyovunwa imeongezeka kutoka shilingi 69 hadi shilingi 130, huku mapato ya kitaifa kutokana na mauzo ya kahawa nje ya nchi yakiongezeka mara mbili kutoka shilingi bilioni 26 hadi bilioni 52.

Alisema ufanisi huo umetokana na mageuzi yaliyofanywa katika mifumo ya usimamizi, uuzaji na malipo ya kahawa, hatua zinazolenga kuhakikisha wakulima wanapata sehemu kubwa zaidi ya mapato yanayotokana na mazao yao.

Rais alisema tayari shilingi bilioni 15.07 zimelipwa kwa wakulima 680,000, akisisitiza kuwa serikali inalenga kuboresha maisha ya wakulima kwa kuhakikisha wananufaika zaidi na thamani ya kahawa wanayozalisha.

Wakati huohuo Rais ametetea mageuzi yaliyofanywa na serikali yake katika sekta ya kilimo, akisema kupungua kwa bei ya mbolea na kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula kumechangia kupunguza gharama ya maisha huku pia kukiongeza mapato ya wakulima.

Ruto alisema serikali yake imeweka kipao mbele sekta ya kilimo kwa kupunguza gharama za pembejeo za kilimo, kuongeza upatikanaji wa chakula na kuhakikisha wakulima wanapata mapato bora kutokana na mazao yao.

“Uhusiano kati ya gharama za uzalishaji, gharama ya matumizi nyumbani na mapato haujitokezi wazi zaidi popote kama ilivyo katika sekta ya kilimo,” alisema Ruto.

Alisema bei ya gunia la mbolea la kilo 50 imepungua kutoka shilingi 7,500 mwaka 2022 hadi shilingi 2,000 mwaka huu, huku serikali ikisambaza jumla ya magunia milioni 38.5 kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea.

Aidha, serikali imesajili takribani wakulima milioni tisa na kupanua upatikanaji wa mbegu bora, huduma za upimaji wa afya ya udongo pamoja na huduma za ugani ili kuboresha uzalishaji wa kilimo nchini.

 

 

Our Correspondent Avatar