, ,

ACT Wazalendo kujadili hali ya kisiasa nchini

Asia Gamba Avatar

Chama cha ACT-Wazalendo kinatarajia kufanya kikao cha kawaida cha Kamati Kuu kwa siku mbili, Novemba 27 na 28, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, kikilenga kutathmini hali ya kisiasa nchini na mwenendo wa shughuli za chama hicho.

Taarifa iliyotolewa leo Novemba 24, 2026 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo, imeeleza kuwa kikao hicho kitafanyika katika Ukumbi wa Hakainde Hichilema, uliopo katika Jengo la Maalim Seif, Makao Makuu ya chama, Magomeni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya chama, yanayoipa Kamati Kuu jukumu la kusimamia, kutathmini na kutoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa majukumu na shughuli zake.

Katika kikao hicho, Kamati Kuu inatarajia kufanya tathmini ya hali ya kisiasa nchini, ikihusisha Tanzania Bara na Zanzibar.

Pia, itapokea na kujadili taarifa ya Sekretarieti kuhusu ziara mbalimbali zilizofanywa na chama, utekelezaji wa majukumu yake na shughuli za kawaida za taasisi hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kikao hicho kitajadili changamoto zilizojitokeza katika shughuli za chama na kutoa maelekezo yatakayolenga kuimarisha utendaji, ufanisi na utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi kijacho. 

Our Correspondent Avatar