Kesi ya Maofisa saba wa Polisi wanaodaiwa kuua yapigwa tena kalenda

Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa polisi mkoani Mtwara, imeahirishwa kutokana na upelelezi bado unaendelea.

Washitakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya hiyo hii leo ikiwa ni kwa mara ya pili, ambapo kwa mara ya kwanza walipandishwa kizimbani Januari 25,2022 na kusomewa shitaka la mauaji ya kukusudia.

Waliopandishwa kizimbani ni Ofisa Upelelezi Wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Charles Onyango, Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Charles Kisinza na Mkaguzi wa Polisi, John Msuya.

Wengine ni Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi, Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salum Juma Mbalu.

Mapema leo Jumanne, washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo saa 2.57 asubuhi na kufikia saa 3.26 asubuhi kesi hiyo ilikuwa imeshasikilizwa na kuahirishwa.

Wakili wa Serikali Ajuaye Bilishanga Zegeli ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo, kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa tena.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mfawidhi, Lugano Kasebele amabaye anasikiliza kesi hiyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 8, 2022 itakapokuja kutajwa tena.

Inadaiwa kuwa Januari 5, maofisa hao wa polisi walimuua Musa Hamis Hamis (25), mkazi wa Nachingwea mkoani Mtwara.

https://mwanzotv.com/2022/02/08/kesi-ya-maofisa-wa-polisi-yapigwa-kalenda/