Mwanzo Tv

Nairobi Kenya

+254 7

24/7 Customer Support

Mon - Fri: 9:00 - 17:30

Online Media always open

Askofu Niwemugizi amsihi Rais Samia kutokubali kulinganishwa na Mungu.

Askofu wa Jimbo Katoliki  la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi

Askofu wa Jimbo Katoliki  la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi amemsihi Rais Samia Suluhu Hassan kutokubali kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile.

Askofu huyo amesema hayo leo katika sherehe za Jubilee ya miaka yake 25 iliyofanyika wilayani Ngara mkoani Kagera, ambapo Rais Samia Suluhu alikua mgeni rasmi

ā€œNikikuomba uwe na afya njema na uwe mnyenyekevu lakini pamoja na madaraka hayo makubwa uliyonayo usikubali kamwe kulinganishwa na Mungu kwa namna yoyote ile  usikubali.” 

Na kuongeza kuwa “Ninakumbuka sana Hayati Benjamini Mkapa najua huko mlikuwa mmezoea mtukufu rais, mtukufu rais alifika mahali akawa mkali kabisa mtukufu ni Mungu tu naomba hilo liwe neno kwako, “ amesema Askofu Niwemugizi.

Aidha Askofu Niwemugizi amemuombea rais Samia katika majukumu aliyokuwa nayo aweze kukuza upendo, kukuza haki na demokrasia nchini ili kuondoa mifarakano

“Basi nakuombea Mungu akusaidie kukuza upendo kati ya Watanzania unaotuongoza,  ukuze haki nayo haki izae amani na utulivu na kukuza demokrasia katika nchi yetu.”

ā€œUkuze upendo na mshikamo wa Watanzania ili hatimaye utumishi wako utukuke na kuacha alama itakayoonwa kwa vizazi vingi.

Mungu akujalie hekima na uvumilivu wa kusikiliza hata yale yanayokela masikio yako,  unajua sisi watoto wako tuko wakorofi, Mungu akujalie tu hekima na uvumulivu hasa pale unapokuwa ni ushauri wenye nia njema ya kulijenga Taifa letu liendelee kuheshimika ndani na nje.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Samia Suluhu ameahidi kutokuwa na tabia ya umungu mtu na kukataa kutukuzwa kwani mara zote amekuwa akishi kwa kujishusha ili awe sawa na wengine.

“Baba Askofu umeniasa mambo ya kukataa kutukuzwa na mimi nataka nikuahidi kwamba hiyo si tabia yangu, ninajitahidi kujishusha niwe sawa na wengine, maana utumishi huu kama mipango ya Mungu ilivyo ameniweka hapa niwatumikie,”- Amesema Rais Samia Suluhu.

Na kuongeza kuwa “Nitajitahidi na Mungu anisaidie kuwa na hekima na uvumilivu na niwe na sikio la kusikiliza yale yanayosemwa na wengine,”-

Askofu Severine Niwemugizi amezaliwa Juni 3,1956 na ni Askofu  Mkatoliki nchini Tanzania.

Aliwekwa wakfu na Askofu Mkuu Anthony Peter Mayala mwaka wa 1997. Tangu mwaka huo, ni askofu wa Jimbo la Rulenge lililopo Ngara mkoani Kagera na pia ni Mkurugenzi wa Radio Kwizera iliyopo huko Ngara.

Aliwahi pia kuwa rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2006.