, ,

Gachagua na Linda Mwananchi Wakutana: Nini Kinapikwa?

Victor Kayanda Avatar

Wafuasi wa upinzani nchini Kenya wanapoendelea kusubiri kwa hamu na ghamu kwa viongozi wa upinzani kumtangaza atakayekabiliana na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao, kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, amekutana na kiongozi wa Linda Mwananchi Seneta Edwin Sifuna katika makazi yake ya Wamunyoro kaunti ya Nyeri.

Mkutano huo umejiri saa chache baada ya Gachagua kurejea nchini Kenya kutoka Marekani alikokuwa kwa takriban miezi miwili.

Gachagua akizungumza katika mkutano huo, alitoa wito wa ushirikiano miongoni mwa viongozi wote wa upinzani akisisitiza kuwa hiyo ndio njia ya pekee ya kuhakikisha kwamba wanamuondoa Rais Ruto uongozini katika uchaguzi wa mwaka wa 2027. Kiongozi huyo ambaye ameonekana kuwa ushawishi mkubwa eneo la Mlima Kenya ametupilia mbali madai kuwa yeye ni kiongozi anayeeneza chuki na ukabila nchini.

“Watu wengine wanatubandika majina lakini hatuko jinsi wanavyotusemea. Mtu asije akawaambia kwamba sisi ni wakabila kwa kuwa wakati tulipomuunga mkono Rais Ruto tulifahamu fika kuwa alikuwa Mkalenjini, tulijua hakuwa Njoroge wala Kamau na tulimuunga mkono,” alisema Gachagua.

Mkutano huo pia unajiri wakati ambapo wanasiasa wanaendelea kubuni miungano ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, huku Gachagua akikutana na viongozi wanaohusishwa na mrengo wa Linda Mwananchi.

Wandani wa Gachagua akiwemo Naibu Kinara wa DCP Cleophase Malala wamekuwa wakipigia upatu Muungano Vuguvugu la Linda Mwananchi chini ya Uongozi wa Sifuna na Chama chao cha DCP ili kuona kwamba upinzani unakuwa nguvu zaidi.

Viongozi wa upinzani wamekuwa wakiraiwa kuungana ili kuhakikisha kuwa wanapata uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wengi ndiposa mgombea wa upinzani aweze kushinda kwa kura nyingi.

Hata hivyo kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Gitile Naituli, iwapo jamii ya Mulembee itaungana nyuma ya Edwin Sifuna na kushirikiana na wenyeji wa Mlima Kenya basi tiketi ya Sifuna na kiongozi mwingine yeyote kutoka eneo la Mlima Kenya litaibuka na ushindi.

“Ikiwa Edwin Sifuna ataungwa mkono na wakazi wa Magharibi hadi mwisho jinsi imebainika kuwa ana ufuasi mkubwa kutoka eneo hilo na aungane na viongozi wa Mlima Kenya basi ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema Prof Naituli.

Edwin Sifuna ameonekena kuwa mkakamavu katika kujinadi kwa wakenya kwa kufanya mikutano ya hadhara ambayo imekuwa ikipokelewa vyema maeneo mbalimbali nchini hatua ambayo imeendelea kumuongezea umaarufu.

Kwa upande mwingine Gachagua alirejea nchini baada ya kuzuru maeneo mbalimbali ya Marekani, yakiwemo Spokane katika jimbo la Washington, Portland katika jimbo la Oregon, Kansas, Dallas katika jimbo la Texas na Boston katika jimbo la Massachusetts.

Akiwa Marekani, aliyekuwa Naibu Rais alikutana na Wakenya wanaoishi ughaibuni, katika ziara ambayo alisema ilikuwa na nafasi ya kutafakari kuhusu mustakabali wake wa kisiasa bila kuathiriwa na maoni ya washirika wake.

Kabla ya kuondoka nchini, Gachagua alikuwa amesema anapanga kukaa Marekani kwa muda mrefu ili kufanya maamuzi muhimu ya kisiasa akiwa mbali na kile alichokitaja kuwa ushawishi usiofaa kutoka kwa washirika wake.

Alisema kuwa akiwa nchini Kenya, hukabiliwa na maoni tofauti kutoka kwa wenzake, hali ambayo, kwa maelezo yake, inaweza kuathiri maamuzi yake.

“Nitakaa huko kwa muda, na kuna sababu. Kuna mambo ninayopanga ambayo hayawezi kupangwa nikiwa hapa,” alisema Gachagua.

Aliongeza kuwa kutokuwa karibu na washirika wake wa kisiasa kungempa nafasi ya kutafakari na kufanya maamuzi kwa uhuru zaidi.

“Wakati niko hapa, kuna ushawishi mwingi. Kaguchia ananiambia jambo hili, Methu lile; huyu ananivuta upande mmoja na mwingine upande tofauti. Ninataka kufanya maamuzi bila ushawishi usiofaa,” alisema.

Hata hivyo, haijabainika mara moja ikiwa mkutano wake na Sifuna ulihusu mipango maalum ya ushirikiano wa kisiasa au mikakati ya pamoja kuelekea uchaguzi wa 2027.

 

Our Correspondent Avatar