, ,

Kalonzo akutana na Gachagua Wamunyoro kwa mashauriano kuelekea uchaguzi wa 2027

Victor Wanaswa Avatar

Kiongozi wa chama cha Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka amekutana na mwenzake wa Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua nyumbani kwake eneo la Wamunyoro kaunti ya Nyeri.

Mkutano huo umewaleta pamoja viongozi hao wakuu wa upinzani wakati ambao miungano ya kisiasa yameendelea kuangaziwa kwa kina kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana na viongozi wengine wenye azma sawia ya kumtoa Rais William Ruto uongozini katika uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 10, 2027.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja Gavana Wavinya Ndeti wa Machakos, Gavana Mutula Kilonzo Junior wa Makueni, Gavana wa kitui Julius Malombe pamoja na Seneta wa kaunti hiyo Enock Wambua.

Upande wa DCP ukiwakilishwa na Seneta John Methu wa Nyandarua, Mbunge Mark Mwenje wa Embakasi Magharibi, Amos Mwago wa Starehe, James Gakuya wa Embakasi North, Mbunge wa EALA Kanini Kega na aliyekuwa Mbunge wa Starehe Maina Kamanda.

Mkutano huo umeandaliwa katika juhudi za kuimarisha muungano wa upinzani ulioimara na tayari kumtoa mwaniaji mmoja atakayemkabili Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

Mazungumzo hayo yamejiri kukiwa na tofauti za kimtazamo miongoni mwa viongozi hao wa upinzani kuhusu azma ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ya kuwania urais. Kiongozi wa DCP tayari alikuwa amekutana na kikosi cha Linda Mwananchi kikiongozwa na Seneta Sifuna tarehe 20 Oktoba na kuibua madai ya uwezekano wa ushirikiano kati ya makundi hayo mawili.

Kulingana na Gachagua, mazungumzo yake na Kalonzo yalilenga kujadili mustakabali wa kisiasa wa Kenya pamoja na kubuniwa kwa serikali mpya itakayoingia mamlakani baada ya uchaguzi mkuu.

“Tulifanya mazungumzo yenye tija na yaliyolenga kujadili jinsi ya kuikomboa nchi yetu na kubuni utawala unaowajali wakenya,” alisema Gachagua.

Vyama vya upinzani vinaendeleza juhudi za kuunganisha wafuasi wao na kufikia mwafaka kuhusu mkakati wa pamoja wa kisiasa kabla ya kampeni za uchaguzi kuanza rasmi.

Naibu kiongozi wa chama cha DCP, Cleophas Malala, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Gachagua na Sifuna, akisema hatua hiyo itaunganisha viongozi kutoka misingi tofauti ya kisiasa na hivyo kuimarisha upinzani.

Kwa mujibu wa Malala, chama cha DCP tayari kimemteua Sifuna kuwa mgombea wake anayempendekeza, na kinaendelea kuwafikia viongozi wengine wa upinzani ili kujenga mwafaka kuhusu azma yake ya kuwania urais.

“Mmemuona kiongozi wa DCP, Rigathi Gachagua, akikutana na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, siku chache zilizopita. Wameungana,” alisisitiza Malala.

 

Our Correspondent Avatar