Serikali ya Kenya imethibitisha kisa cha tatu cha ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo, huku watu 127 waliokuwa na mawasiliano ya karibu na wagonjwa wakiwekwa karantini katika juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Wizara ya Afya ilisema Ijumaa, Oktoba 16, kuwa mgonjwa wa tatu ni mwanamke mwenye umri wa miaka 65 ambaye alikuwa amewekwa karantini tangu Oktoba 6 baada ya kutambuliwa kuwa miongoni mwa watu waliokuwa na mawasiliano ya karibu na wagonjwa wa kwanza na wa pili.
Mwanamke huyo alianza kuonyesha dalili za homa, maumivu ya koo na kujihisi dhaifu akiwa karantini, hali iliyowafanya wahudumu wa afya kumtenga na kumfanyia vipimo vya kuthibitisha ugonjwa huo.
Sampuli zake zilipimwa na kupatikana na virusi vya Ebola katika maabara ya kitaifa ya marejeleo ya virusi pamoja na maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu nchini Kenya (KEMRI).
Mgonjwa huyo amehamishiwa katika kitengo cha kutibu magonjwa ya kuambukiza, ambako anapatiwa huduma za matibabu na uangalizi na wahudumu wa afya waliofunzwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Afya, Dkt. Patrick Amoth, alisema kutambuliwa mapema kwa mgonjwa huyo kutokana na kuwekwa karantini kunampa nafasi nzuri zaidi ya kupata nafuu na kupunguza hatari ya kuwaambukiza watu wengine.
Wizara hiyo iliongeza kuwa mgonjwa wa pili alikuwa katika hali tulivu na akiendelea kuimarika kutokana na matibabu anayopokea.
Kisa hicho kipya kimegunduliwa ndani ya mfumo wa karantini, hatua ambayo mamlaka za afya zinasema imesaidia kumtambua na kumtenga mgonjwa kabla ya kusababisha maambukizi zaidi.
Hata hivyo, serikali imesisitiza kuwa hatari ya maambukizi kwa umma kwa sasa ni ndogo, huku kukiwa hakuna ushahidi wa ugonjwa huo kuanza kuenea katika jamii.
Kufikia Oktoba 16, maafisa wa afya walikuwa wametambua watu 130 waliokuwa na mawasiliano na wagonjwa, ambapo 127, sawa na asilimia 97.7, walikuwa wamefikiwa na kuwekwa karantini. Juhudi za kuwatafuta watu watatu waliosalia zilikuwa zikiendelea.
Wizara ilisema kiwango hicho cha ufuatiliaji kimevuka kigezo cha kimataifa cha asilimia 85 kinachochukuliwa kuwa muhimu katika kukabiliana na maambukizi.
Mamlaka za afya zimeonya kuwa visa zaidi vinaweza kugunduliwa miongoni mwa watu waliowekwa karantini kabla ya kipindi chao cha ufuatiliaji kukamilika, lakini zimesisitiza kuwa wagonjwa watatambuliwa na kupatiwa matibabu kwa haraka.
Katika hatua za kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo, serikali imesambaza vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi, vifaa vya kudhibiti maambukizi hospitalini na vifaa vya uchunguzi wa afya ya umma katika kaunti 28 zilizo katika hatari kubwa pamoja na maeneo ya kuingilia nchini.
Wasafiri wanaoingia nchini kutoka mataifa 10 yaliyotambuliwa kuwa katika hatari kubwa pia watatakiwa kujaza fomu ya kidijitali ya ufuatiliaji wa afya kabla ya kupanda ndege na kuwasilisha msimbo wa QR kwa maafisa wa afya bandarini wanapowasili.








