Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome amethibitisha kupunguzwa kwa usalama wa aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Koome alisema kuwa mkuu wa kikosi cha usalama cha Uhuru aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na afisa wa cheo cha chini.
“Afisa huyo atapewa majukumu ya amri yanayolingana na cheo chake,” alisema.
Inspekta Jenerali alitupilia mbali madai yoyote kwamba uamuzi huo ulichochewa kisiasa.
“Hakuna siasa katika hili na Inspekta Jenerali hatakubali kuingizwa kwenye siasa,” alisema Koome.
Siku ya Alhamisi, duru za habari zilidai kuwa idadi ya maafisa waliotumwa kwa rais huyo wa zamani imepunguzwa kutoka 96 hadi 25, huku maafisa wa usalama wanaohusishwa na wanafamilia wengine pia wakiondolewa.
Koome alithibitisha mabadiliko katika usalama wa makatibu wa zamani wa baraza la mawaziri lakini hakutaja majina yoyote.
“Je, unampa Katibu wa Baraza la Mawaziri mstaafu usalama sawa na yule aliye ofisini ambaye lazima awe ofisini kufikia saa 12 asubuhi?” aliuliza Koome.
Sheria ya Mafao ya Rais inaeleza kuwa rais mstaafu ana haki ya kuwa na walinzi sita na ulinzi wa kutosha katika makazi yao ya mijini na vijijini, ambayo yatapitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa. Hata hivyo, sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2013 ili kuondoa ukomo wa juu zaidi, ikizingatiwa kwamba kutumwa kwa wanausalama kutakuwa kama ilivyothibitishwa na waziri mwenye dhamana ya usalama wa taifa kwa kushauriana na rais mstaafu.