,

Mlinzi wa Zamani wa Raila Aeleza Dakika za Mwisho Kabla ya Kifo Chake

Victor Wanaswa Avatar

Aliyekuwa mlinzi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, Maurice Ogeta amesimulia matukio ya dakika za mwisho kabla ya kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe akisema aliona ishara zilizomfanya kuhisi kuwa hali haikuwa shwari hospitalini.

Ogeta amesema kuwa kabla ya kupokea taarifa za kifo cha Raila Oktoba 15, 2025, aliona maandalizi ya vifaa vya maombi na mishumaa. Alipomuuliza daktari aliyekuwa akimhudumia Raila, Dkt. Oluoch Olunya kuhusu kilichokuwa kikiendelea alielezwa kuwa maombi yalikuwa sehemu ya huduma za kawaida katika hispitali hiyo ya kimishenari.

Hata hivyo, Ogeta amesema maelezo hayo hayakumwondoa hofu na wasiwasi kutokana na ishara nyingine alizokuwa akiziona.

Akizungumza katika mahojiano na vituo vya televisheni nchini Kenya, Ogeta amesema alihisi wazi kuwa hali haikuwa sawa.

Kuhusu kilichotokea wakati Raila alipoanza kuugua, Ogeta alisema aliyekuwa Waziri Mkuu alikuwa akifanya matembezi yake ya kawaida ndani ya hospitali, akipanga kukamilisha mizunguko mitano katika njia yenye urefu wa takriban mita 50.

Hata hivyo, baada ya kuanza mzunguko wa kwanza Raila alisimama ghafla na kutoa sauti ya mshangao, hali iliyomfanya Ogeta kumuuliza iwapo alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo au mguu.

Mlinzi huyo wa muda mrefu wa Raila aidha, amesema alikuwa umbali wa takriban mita moja kutoka kwa Raila wakati tukio hilo lilipotokea.

Kwa mujibu wa Ogeta, Raila alionekana kama mtu aliyepigwa na butwaa akitazama kana kwamba kuna kitu mbele yake ambacho hakuwa akikion. Ogeta alijaribu kumshawishi ampelekea kwenye kiti ili aweze kumchunguza lakini hali hiyo ilizua wasiwasi mkubwa kwake.

Aidha, Ogeta amefafanua kuwa video inayomuonyesha Raila akiwa amevalia joho jeupe na kutembea kwenye hospitalini huku akimfuata kwa karibu, haikurekodiwa muda mfupi kabla ya kifo chake bali wakati wa upasuaji wake wa kwanza mjini Dubai.

Rails Odinga alifariki dunia Oktoba 15, 2025, akiwa na umri wa miaka 80 alipokuwa akipokea matibabu nchini India. Alikuwa Waziri Mkuu wa Kenya kuanzia mwaka 2008 hadi 2013 na alikuwa mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi katika historia ya kisiasa ya nchi hii.

Kwa miongo kadhaa, Raila alishiriki kikamilifu katika siasa za upinzani, harakati za mageuzi ya kikatiba uchaguzi mbalimbali wa urais.

 

Our Correspondent Avatar