Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amepokea orodha ya majina ya awali ya kaya 86 zenye watu 453 ambao wamekubali kuondoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro nchini humo kwa hiari huku wengine wakiendelea kujiandikisha.
Taarifa iliyotolewa Machi 10, 2022 na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema kuwa, Majaliwa amepokea majina hayo baada ya kumaliza kikao na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai (Laigwanak) kwenye mkutano uliofanyika eneo la Oretei Loongaik-Marya, kwenye Chuo cha Ufundi Arusha, jijini Arusha.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mazungumzo ambayo Waziri Mkuu aliyafanya na wadau wa uhifadhi kwenye vikao vilivyofanyika Februari 14 na 17 mwaka huu kwenye tarafa za Loliondo na Ngorongoro, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.
Majina hayo yamekabidhiwa kwa Waziri Mkuu na Mkuu wa Mkoa wa Arusha (DC), John Mongela na tayari yalishahakikiwa mara baada ya wakazi hao kujiandikisha.
“Tutawasimamia vizuri hadi waende kule wapate hati za mashamba, nyumba na maeneo ya kulisha mifugo yao.”
Akizungumza na Malaigwanak hao zaidi ya 350, Waziri Mkuu amesema Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara mkoani humo aliwaambia kuwa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro iko hatarini ya kutoweka ndani ya muda mfupi na akatoa maagizo viongozi waende kuwasikiliza wananchi juu ya hatua za kuchukua ili tunu hiyo isipotee.
“Ile hatari aliyosema Rais ni ipi? Zamani watu waliweza kuishi na wanyama bila tatizo kwa sababu kulikuwa na wakazi 8,000 tu wenye ng’ombe 20 hadi 30. Leo hii kuna wakazi 110,000 na mifugo zaidi ya 813,000 wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo”
“Zamani maboma yalikuwa yamesambaa lakini leo hii nyumba zimejaa, tena za bati na tofali. Idadi ya watu imeongezeka, idadi ya mifugo imeongezeka na makazi yameongezeka. Hakuna huduma za afya au shule wakati ni hitaji muhimu kwa wananchi.” imesema taarifa hiyo
Amewaeleza viongozi hao kwamba Serikali imetenga eneo la kilometa za mraba 400,000 wilayani Handeni ambalo kati ya hizo, kilometa za mraba 220,000 zilitumika kwa kujenga nyumba, kupima viwanja na kutenga maeneo ya malisho.
“Tumepima viwanja 2,406 ambapo kati ya hivyo, viwanja 2,070 tumeandaa kwa ajili ya makazi na kila kimoja kina ukubwa wa ekari tatu. Tumeanza na nyumba za kuanzia 101 za vyumba vitatu vya kulala kwa wale wanaotaka. Tuna viwanja 336 kwa ajili ya huduma kama shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya. Ujenzi wa mifumo ya maji kazi inaendelea
Taarifa hiyo imesema kuwa Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Wamasai Tanzania, Isack Ole Kisongo alisema kwa nafasi yao viongozi wa kimila wako tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote.
“Kwa kunyanyua rungu zetu tumekula kiapo kwa kukubali kuwa Ngorongoro na hifadhi nyingine nchini zilindwe kwa nguvu zote ili hadhi yake irudi kama zamani” imesema taarifa hiyo ikimnukuu kiongozi wa Wamasai nchini
Laigwanani wa Malaigwanani wa Ngorongoro, mzee Matengway Ole Tauwo alimweleza Waziri Mkuu kwamba anasubiri tarehe ya kuhamia huko kwa sababu ameenda hadi Handeni na ameona kwa macho yake kwamba mipango ya Serikali ina lengo zuri.