Watiwa mbaroni wakiwa na kilo 60 za bangi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watuhumiwa 19 kwa kujihusisha na matukio ya uhalifu huku likifanikiwa kukamata vitu na vielelezo mbalimbali ikiwemo silaha aina ya Chinese Pistol yenye namba 071T4823 ikiwa na risasi tano, pikipiki 4, baiskeli 2 na mafuta aina ya Diesel lita 60 na Petrol lita 20 Vitu vingine ni Dawa za kulevya aina ya Bangi kilo 60 na gramu 540, Mirungi bunda 58, Heroine kete 166, Television 2, Godoro 1, Subwoofer 1 na CPU 1.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema watuhumiwa hao na vitu hivyo vimekamatwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia tarehe 28/05/2023 hadi tarehe 21/06/2023 kupitia misako na doria mbalimbali.

Ameeleza kuwa katika kipindi hicho kesi mbalimbali ziliweza kufanikiwa mahakamani ikiwemo kesi moja ya mauaji ambapo mtuhumiwa alihukumiwa kunyongwa hadi kufa, kesi moja ya kujaribu kubaka ilihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na nyingine mbili za kubaka zilihukumiwa kifungo cha miaka 30 Jela kila moja.

“Pia kesi moja ya kumpa mimba mwanafunzi mtuhumiwa alihukumiwa kifungo cha miaka 30 Jela na kesi moja ya kutorosha mwanafunzi ilihukumiwa kifungo cha miaka 30 Jela”amesema Kamanda Magomi.

Amezitaja kesi zingine zilizopata mafanikio ni pamoja na kujeruhi ambayo ilihukumiwa kifungo cha miaka 30 Jela, kujifanya mtumishi wa Serikali miaka 02 Jela, kuvunja nyumba usiku ilihukumiwa miaka 05 Jela na wizi wa gari ilihukumiwa miaka 03 Jela.