Watu wanne wafariki kwenye ajali Tanga

Watu wanne wamefariki dunia na wengine 37 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili wilayani Handeni mkoani Tanga.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia leo Jumatano Machi 16, 2022 katika Kijiji cha Sindeni, Wilayani Handeni mkoani Tanga, ambapo ilihusisha basi ndogo ya abiria aina ya Coaster ambayo iliigonga Toyota Hiace na watembea kwa miguu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga (RPC), Safia Jongo, watu wanne walifariki huku wengine 37 wakijeruhiwa.

“Chanzo cha ajali hii ni gari aina ya Isuzu Jorney ikitokea Tanga mjini kwenda Handeni, iligonga watembea kwa miguu na gari ambayo iliharibika njiani ambapo watu watatu walifariki hapohapo na mmoja alifariki hospitali akiwa anapatiwa matibabu huku saba wakijeruhiwa sana na wengine wamepata michubuko ” amesema Kamanda Jongo

Mganga mkuu Hospitali ya mji Handeni, Dkt Hudi Shehdadi amesema kuwa walipokewa majeruhi 38 ambapo mmoja alifariki dunia akiwa bado anapatiwa matibabu.

Wengi wa majeruhi wa ajali hiyo ni wananchi wa kijiji cha Sindeni ambao walijitokeza kwaajili ya kushuhudia ajali ya kwanza,ambapo lilitokea basi lingine na kuwagonga wakiwa eneo la tukio.