Fahamu zaidi kuhusu kirusi kipya cha UVIKO 19- Omicron

visa vya kirusi cha Omicron sasa vipo katika zaidi ya nchi 20 na katika mabara yote

0

Omicron ni kirusi cha UVIKO-19 kilichotangazwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini na visa vya kirusi hicho sasa vipo katika zaidi ya nchi 20 na katika mabara yote. Kilipewa jina Omicron wiki moja tu iliyopita na itachukua muda kuelewa athari zake kwenye janga hili.

Huu hapa ni muhtasari kuhusu kirusi cha Omicron.

Kirusi cha Omicron kilitokea wapi?

Hatujui. Mtaalamu wa magonjwa wa Afrika Kusini Salim Abdool Karim anasema kiligunduliwa kwanza nchini Botswana na kisha Afrika Kusini ambapo tangazo kuhusu kirusi hicho kipya lilifanywa mnamo Novemba 25.

Siku ya Jumanne mamlaka ya Uholanzi ilitangaza kwamba siku sita kabla ya hapo Novemba 19 mtu mmoja alikuwa amepimwa na kukutwa na kile ambacho pia kiligeuka kuwa kirusi cha Omicron.

Walakini, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema “kisa cha kwanza kilichothibitishwa na maabara kilitambuliwa kutoka kwa sampuli iliyokusanywa mnamo 9 Novemba 2021,” bila kutaja kutoka wapi.

“Pengine kimekuwa kikienea Afrika Kusini kwa muda mrefu kuliko tulivyofikiria – tangu mapema mwezi Oktoba,” Jean-Francois Delfraissy, rais wa bodi ya ushauri ya kisayansi ya serikali ya Ufaransa aliiambia AFP.

Kwa nini ni “kimezua wasiwasi”?

Siku moja baada ya tangazo la Afrika Kusini WHO ilikipa kirusi hicho herufi ya lugha ya Kigiriki, kama vile virusi vya awali na ikaainisha kuwa ni kirusi “cha kutia wasiwasi.”

Uainishaji unatokana na sifa za kijeni za Omicron na pia jinsi kinavyoonekana kuathiri watu kufikia sasa.

Kulingana na utafiti kirusi hiki kinaambukiza zaidi na ni vigumu zaidi kukidhibiti kupitia chanjo za sasa – lakini uwezekano huu ni wa kinadharia hadi sasa.

Wakati huo huo, visa vya kirusi hiki katika jimbo la Gauteng la Afrika Kusini, linalojumuisha Johannesburg, zimeongezeka kwa kasi huku wengi wakitambuliwa kuwa na kirusi cha Omicron.

Watafiti kote duniani wanachunguza jinsi Omicron inavyoambukiza, athari kinachosababisha, na ikiwa ni sugu zaidi kwa chanjo. WHO imesema mchakato huo huenda ukachukua wiki kadhaa.

– Je kitachukua nafasi ya kirusi cha Delta?

 Kirusi cha Delta kwa sasa ndiyo aina ya UVIKO ambayo imeenea zaidi kote duniani.

Virusi vingine ambavyo viliibuka baada ya Delta (kama vile Mu na Lambda) havijaweza kuathiri idadi kubwa ya watu –lakini kuenea kwa Omicron huko Gauteng kunaonyesha huenda kikaathiri watu zaidi.

Siku ya Alhamisi Kituo cha Ulaya cha Kudhibiti Magonjwa (ECDC) kilisema kwamba ikiwa kirusi cha Omicron kitaenea barani Ulaya jinsi kinavyoenea Afrika Kusini, Omicron inaweza kusababisha visa vingi vya UVIKO 19 ndani ya miezi michache.

Walakini, Delta haikuwepo sana Afrika Kusini, kwa hivyo kulinganisha jinsi kinavyoenea Afrika Kusini na Uropa katika hatua hii ni vigumu kufanya.

Akiandika katika gazeti la kila siku la Uingereza la The Guardian, mtaalam wa Amerika Eric Topol alisema haijathibitishwa iwapo kuenea kwa Omicron ni kwa sababu ya “maambukizi makubwa, kama Delta, au kwasababu kinakwepa kinga.”

Ukwepaji wa kinga ni wakati virusi vinaweza kumwambukiza mtu ambaye tayari amepata kinga kutoka kwa maambukizi ya awali au kutoka kwa chanjo.

– Je kirusi hiki ni hatari zaidi?

Siku ya Jumapili, daktari wa Afrika Kusini alisema ametibu takriban visa 30 vya Omicron na alikuwa amekumbana na “dalili chahce” kwa wagonjwa hao.

Jumuiya ya wanasayansi ilionya dhidi ya kutoa hitimisho kulingana na ushuhuda huu kwani wagonjwa walikuwa wachanga zaidi na kwa hivyo hawakuwa katika hatari kubwa ya UVIKO.

Kufikia sasa, visa vyote vilivyogunduliwa huko Uropa ni “visivyo na dalili au venye dalili chache,” kulingana na EDCD.

Hii haimaanishi kuwa Omicron haitasababisha madhara makubwa ya UVIKO – lakini inaacha nafasi wazi kwa nadharia ya matumaini isiyo ya kawaida.

“Ikiwa Omicron inaambukiza sana lakini haisababishi UVIKO yenye madhara makubwa inaweza kutoa kinga ya kikundi na kuchangia kufanya SARS-CoV-2 kuwa virusi vya msimu, ambavyo vinaweza kusaidia kumaliza janga hili,” Mtaalamu wa magonjwa ya virusi Mfaransa Bruno Canard alitweet.

Aliongeza, hata hivyo, kwamba hali kama hiyo itakuwa “bahati sana.”

Nafasi ya chanjo?

Tena, ni mapema mno kusema kama chanjo zitakuwa na ufanisi dhidi ya maambukizi au ugonjwa  kutoka kwa Omicron kuliko dhidi ya virusi vingine.

“Tunapaswa kuona iwapo kingamwili zinazozalishwa na chanjo za sasa bado zinafanya kazi na kwa kiwango gani – kama bado zinazuia athari za kirusi hicho,” alisema Enouf.

Lakini hata kama chanjo hazifanyi kazi vizuri dhidi ya Omicron haimaanishi kuwa hazitafanya kazi kabisa. Mbali na mwitikio wa kingamwili ambao unaweza kudhoofishwa na mabadiliko katika Omicron, mwili una seli za T ambazo zinaweza kuulinda dhidi ya makali ya Omicron. “Tunafikiri kwamba nguvu ya seli za mwilini zitakuwa na ufanisi dhidi ya Omicron,” Delfraissy alisema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted