Ng’ombe 35,746 wafariki kwa ukame Simanjiro

Hali hiyo imetajwa kusababishwa na ukosekanaji wa maji na malisho uliovikumba vijiji vya wilaya hiyo.

0

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Sendeu Laizer amesema Ng’ombe wapatao 35,746 wamekufa wilayani humo kutokana na ukame uliovikumba vijiji vya wilaya ya Simanjiro.

Sedeu amesema mbali na Ng’ombe ipo mifugo mingine iliyokufa kutokana na ukame huo ambapo amebainisha kuwa takribani mbuzi 10,033 wamekufa, Kondoo 15,136, na Punda 1670, hali inayofanya jumla ya mifugo iliyokufa wilayani humo kufikia  62,593

Hayo aliyabainisha kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo na kusema kuwa katika kipindi hiki hali ya mifugo katika maeneo mengi ya Simanjiro siyo ya kuridhisha kutokana na uhaba wa maji na malisho.

Amesema ufuatiliaji na ukusanyaji wa taarifa za vifo vya mifugo kutokana na athari za ukame unaendelea katika vijiji vyote.

“Hali hii imesababisha baadhi ya mifugo kufa na wafugaji wengi kuhama na kurundikana katika maeneo machache yenye maji na malisho,” amesema Sendeu.

Wakati Sendeu akisema hayo Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema kutokana na ukame huo jamii nyingi zimeingia kwenye umaskini kutokana na mifugo yao kufa.

Ole Sendeka amesema kwa sababu ya ukame uliopo nchini baadhi ya wafugaji wamehamisha mifugo yao nje ya nchi ili ipate malisho.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted