Nani kumrithi Maalim Seif Sharif Hamad

Harakati za kumtafuta mrithi wa kiti cha Uenyekiti ilioachwa na Maalim Seif hivi sasa zinaendelea ndani ya chama cha ACT-Wazalendo

0
Aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, marehemu Maalim Seif Sharif Hamadi

Chama cha ACT- Wazalendo hadi sasa bado hakijapata mrithi wa kiti cha Uenyekiti wa chama hicho nafasi ambayo iliachwa na  Maalim Seif Sharif Hamadi baada ya umauti kumfika.

Kwa sasa chama hicho kimeitisha Mkutano Mkuu utakaofanyika Januari 29 ambapo ndipo itajulikana ni nani atarithi mikoba hiyo.

Wanaowania kiti hichi ni aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji pamoja na waziri wa zamani, Masoud Hamad Masoud ndio wagombea pekee waliojitokeza kutaka kurithi kiti cha hicho. 

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Joram Bashange alitoa taarifa hiyo jana wakati alipozungumza na wanahabari juu ya maandalizi ya Mkutano Mkuu huo.

Bashange alisema mpaka kazi ya uchukuaji na urudishaji fomu inafungwa juzi, wanachama 11 walijitokeza kutaka kujaza nafasi zilizoachwa wazi ikiwemo ya Mwenyekiti kutokana na kifo cha Maalim Seif aliyefariki dunia Februari 17, mwaka jana.

Alisema mchakato wa kujaza nafasi hizo ulianza Januari 4 ikiwa ni uchukuaji wa fomu na urejeshaji wa fomu hizo na kuhitimishwa juzi Januari 17, mwaka huu ambapo jumla ya wagombea waliojitokeza kutaka kujaza nafasi tatu ni 11.

Alisema nafasi zinazotakiwa kujazwa ni ya Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti wa Taifa kutoka upande wa Zanzibar na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nafasi moja. Aliongeza kuwa kwa nafasi ya Mwenyekiti Taifa, waliojitokeza ni wawili ambao ni Juma Duni Haji kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja na Masoud Hamad Masoud kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba.

“Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Taifa ambayo ni nafasi inayotakiwa kujazwa na mtu kutoka Zanzibar, ina wagombea wawili ambao ni Othman Masoud Othman kutoka Kaskazini Pemba na Juma Saidi Saanani kutoka Mjini Magharibi Unguja,” alisema Bashange.

Kwa upande wa nafasi moja ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu inagombewa na wajumbe kutoka Tanzania Bara kwa kuwa mwanachama aliyefariki anatoka Bara, ina wagombea saba ambao ni Chrisant Joseph Msipi kutoka Shinyanga, Esther Thomas na Fungo Godlove wote kutoka Dar es Salaam, Johnson Mauma kutoka Arusha, Msafiri Mtemelwa na Fidewil Christopher wote kutoka Tabora na Japhet Masawe kutoka Kilimanjaro.

Bashange alisema baada ya kazi ya kurudisha fomu kufungwa, Kamati ya Uchaguzi itakaa leo kuandaa taarifa ya wagombea wote na kuiwasilisha kwa Sekretarieti ambayo nayo itakaa Januari 22 kuandaa kikao cha Kamati Kuu.

Ameongeza kuwa  Kamati Kuu itakaa kikao Januari 27, mwaka huu na kuandaa taarifa na taratibu za kikao cha Halmashauri Kuu itakayokaa Januari 28 na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea na kampeni zitafanyika siku hiyo hiyo kupitia mdahalo wa wazi kisha kuitisha Mkutano Mkuu Januari 29 ili wajumbe wafanye uchaguzi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted