Wasichana na watoto milioni 200 wamekeketwa duniani kote

Ukeketaji hufanyika kwa watoto wa kike wenye umri wa kuanzia pale alipozaliwa hadi umri wa miaka 15 na kwa sababu tofauti tofauti za kijamii kulingana na eneo na...

0

Wakati dunia inaelekea kuadhimisha siku ya kutokomeza ukeketaji  inayofanyika Februari 6 kila mwaka, takribani watoto na wasichana milioni 200 duniani kote wamekeketwa na hii inajumuisha aina zote za ukeketaji unaofanyika kubadili maumbile ya sehemu zao za siri kwa sababu zisizo za kimatibabu.

Kwa kiasi kikubwa ukeketaji  hufanyika kwa watoto wa kike wenye umri wa kuanzia pale alipozaliwa hadi umri wa miaka 15 na kwa sababu tofauti tofauti za kijamii kulingana na eneo na nchi.

Mathalani kwa maeneo mengine wanadai kuwa ni mila muhimu ya kumuandaa mtoto wa kike kwa ajili ya kuingia utu uzima na ndoa. Kwingineko FGM inahusishwa na maadili ya kijamii ya kukamilika kiusichana na kupunguza hamu ya kufanya tendo la ngono.

Wasichana wanaokeketwa hukumbwa na madhara ya muda mfupi kama vile maumivu, mshtuko, kuvuja damu kupiga kiasi na kushindwa kutoa mkojo huku madhara ya muda mrefu ni pamoja na kushindwa kufanya tendo la ndoa, kujifungua kwa tabu na madhara kwa  afya ya akili.

Umoja wa Mataifa  umesema ukeketaji unafanyika katika nchi 30 Afrika na Mashariki ya Kati, na unatekelezwa pia barani Asia na Amerika ya Kusini na kwa baadhi ya jamii za wahamiaji huko Ulaya Magharibi, Amerika Kaskazini, Australia na New Zealand.

Katika baadhi ya nchi, inafanywa katika takribani nchi nzima. UNICEF inasema kuwa asilimia 90 ya wasichana Djibouti, Guinea, Mali na Somalia wamekeketwa.

Shirika la Afya Duniani limetoa taarifa juu ya mwelekeo unaotia shaka wa FGM kutekelezwa na wahudumu wa afya ikisema kuwa takribani msichana 1 kati ya 4 waliokeketwa, amefanyiwa hivyo na mhudumu wa afya, idadi ambayo ni sawa na wasichana na wanawake milioni 52 duniani kote.

Hata hivyo WHO inaonya kuhusu gharama za matibabu kwa wale manusura wa ukeketaji ikisema kuwa gharama ya matibabu kutokana na athari za ukeketaji huenda ikafika dola bilioni 1.4 kimataifa kwa mwaka iwapo mahitaji yote ya kiafya yatashughulikiwa. 

Katika nchi binafsi, gharama hii inakaribia asilimia 10 ya matumizi ya mwaka mzima ya afya kwa wastani ambapo katika baadhi ya nchi idadi hii huenda ikafika asilimia 30.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted