GSM wajiondoa udhamini Ligi Kuu

Hii ni baada ya madai kuwa TFF na Bodi ya Ligi kushindwa kusimamia matakwa yaliyopo kwenye mkataba walioingia

0

Kampuni ya GSM imejiondoa kama mdhamini mwenza wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya mkataba wao kutokwenda kama walivyotarajia.

Ofisa Biashara wa GSM,  Allan Chonjo amesema wamejiondoa kwenye udhamini mwenza wa Ligi Kuu baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) na Bodi ya Ligi kushindwa kusimamia matakwa yaliyopo kwenye mkataba walioingia.

Akizungumza na wanahabari leo, Chonjo amesema waliwaandikia barua TFF  baada ya kuona tofauti ya makubaliano na ilivyo kwenye mkataba.

“Haya hayajawa maamuzi rahisi kwa kampuni ya GSM kwani tunatambua vipo baadhi ya klabu za mpira zitaumizwa pamoja na  wadau mbalimbali na hatua hii haikuwa dhamira yetu kufikia uamuzi huu mgumu,” amesema Chonjo na kuongeza;

 “Upande wa klabu udhamini wa klabu tutaendelea kuwa kwenye mkataba wetu kama kawaida bali tumejitoa upande huu wa Ligi.”

Wakati huohuo Chonjo amesema Ghalib Said ambaye alikuwa kwenye kamati ya Uenyekiti wa kamati ya ushindi ya timu ya Taifa Tanzania amejiondoa kwenye nafasi hiyo  pamoja na nafasi ya ujumbe.

Ikumbukwe kuwa Mkataba wa GSM na TFF ulisainiwa Novemba mwaka jana hivyo umedumu kwa siku takribani 76 tu tangu kusainiwa.

Kampuni wa GSM, iliingia mkataba wa miaka miwili na Ligi Kuu Bara wenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 kama mdhamini mwenza.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted