Waziri ataka bei ya vifaa vya ujenzi na vinywaji kushuka

Amesema wazalishaji, wasambazaji na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi wauze bidhaa kwa kuzingatia gharama halisi za uzalishaji na usambazaji.

0
Dk Ashatu Kijaji, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Serikali ya Tanzania, imewaagiza wazalishaji, wasambazaji na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi pamoja na wa vinywaji baridi washushe bei za bidhaa hizo mara moja, lengo likiwa ni kukabiliana na hali ya mfumuko wa bei unaoendelea hapa nchini.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, nchini humo Dk Ashatu Kijaji alitoa maagizo hayo makao makuu ya nchi jijini Dodoma wakati akitoa  tathmini ya mwenendo wa uzalishaji, usambazaji na bei za vifaa vya ujenzi na bidhaa zingine muhimu.

Dk. Kijaji alisema kwa kipindi kirefu kumekuwa na malalamiko kuhusu upandaji holela wa bei ya bidhaa hasa vifaa vya ujenzi na bidhaa nyingine yakiwemo mafuta ya kula, sukari na uhaba wa vinywaji baridi.  

“Hali hiyo si tu imeendelea kuongeza gharama za maisha kwa Mtanzania mmoja mmoja, lakini pia imeendelea kuathiri uchumi kwa kuongeza gharama za ujenzi wa miundombinu na miradi mingine ya kimkakati,” alisema Dk Kijaji.

Alielekeza wazalishaji, wasambazaji na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi wauze bidhaa kwa kuzingatia gharama halisi za uzalishaji na usambazaji na endapo itabainika wauzaji wanapandisha bei kiholela basi mamlaka husika wa bidhaa hizo wanapaswa kumchukulia hatua za kisheria.

“Kwa kuwa kitendo cha kupanga bei kati ya washindani ni uhujumu uchumi, nazielekeza mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kupanga bei kwa bidhaa kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Dk Kijaji.

Pia alielekeza wazalishaji wazalishe bidhaa hizo kulingana na uwezo wa viwanda uliosimikwa ili kukidhi mahitaji ya soko.

Uchunguzi umebainisha kuwa pamoja na kuwepo viwanda 17 vya saruji bado uzalishaji ni takribani asilimia 58 ya uwezo wa viwanda wakati kwa bidhaa za nondo kuna viwanda 16 vyenye uwezo wa kuzalisha tani 1,082,788 za nondo za ukubwa mbalimbali na kwa sasa uzalishaji hauzidi tani 750,000.

“Tathmini inaonesha kuwa ongezeko holela la bei za vifaa vya ujenzi, hususani saruji na nondo linasababishwa na wazalishaji wa bidhaa husika kufanya uzalishaji banifu na kutokuwa na mfumo wa wazi wa usambazaji wa bidhaa hizo ambapo kuna mnyororo mrefu wa usambazaji wa bidhaa kutoka kiwandani mpaka kumfikia mlaji wa mwisho,” alisema Dk Kijaji

Dk Kijaji pia alizielekeza mamlaka zote za udhibiti kuchukua hatua kali dhidi ya walimbikizaji na wauzaji kupitia mlango wa nyuma wanaosababisha bei za bidhaa kupanda sokoni ili kuhakikisha kuwa bidhaa zinafika sokoni kwa wakati na kwa bei shindani. 

Alisema uchunguzi umebaini kuwapo kwa ucheleweshwaji wa makusudi wa utoaji wa saruji kutoka viwandani kwenda kwa wasambazaji na wanunuzi wa ndani, hususani wale wadogo, waliokwishalipia saruji husika tofauti na wanunuzi wa nje ambao hupatiwa saruji kwa urahisi zaidi. 

“Serikali haitavumilia tabia ya wafanyabiashara wachache kuanzia wazalishaji hadi wasambazaji wenye dhamira ovu ya kuwaumiza wananchi kwa kujiamulia kupandisha bei za bidhaa bila kufuata utaratibu kwa manufaa yao binafsi,” alisema.

Dk Kijaji aliongeza kuwa gharama halisi za uzalishaji wa saruji haiakisiwi katika bei ya saruji iliyopo sokoni ikilinganishwa na uwiano huo katika nchi jirani na kwingineko duniani.

Alisema ongezeko la bei ya saruji na nondo halina uwiano halisi na gharama za usafirishaji na usambazaji na pia haina uhusiano na mwenendo wa nguvu za utashi wa mlaji na ugavi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted