Shahidi akwamisha kesi ya Mbowe kuendelea.

Ni baada ya hali yake kiafya kutoimalika na kumfanya kushindwa kufika mahakamani

0

Kesi ya Freeman Mbowe na wenzake watatu leo imeshindwa kuendelea katika Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, baada ya shahidi kushindwa kufika mahakamani hapo kutokana na afya yake kuteteleka.

Itakumbukwa hapo jana Mahakama hiyo iliahirisha shauri hilo baada ya shahidi huyo wa Jamhuri Askari Polisi Tumaini Swila, kusimama na kuiomba mahakama kuwa anashindwa kuendelea kutoa ushahidi kutokana na kwamba anaumwa hivyo mahakama imruhusu aende hospitali kupata matibabu.

Jaji anaendesha kesi hiyo Joachim Tiganga, akazingatia maombi hayo na kuahirisha kesi hiyo hadi hii leo ambapo shahidi huyo alipaswa kufika akiwa na uthibitisho kutoka kwa daktari ili kuithibitishia mahakama ni kweli alikua anaumwa.

Hii leo Jopo la mawakili wa serikali wameiambia Mahakama kwamba shahidi ameshindwa kufika baada ya daktari wake kumshauri kuwa anatakiwa apumzike kwa muda kutokana na hali yake, kwani hata jana alipotoka mahakamani hapo alipofika hospitalini alipewa mapumziko ya saa kadhaa.

“Mheshimiwa Jaji Shahidi ameshauriwa na Daktari kupumzika na sisi hatuwezi kwenda kinyume na ushauri wa Daktari. Pia tungeweza kutafuta shahidi mwingine wa kuendelea naye ila kwa muda wa jana na leo isingetosha kutafuta shahidi mwingine” amesema wakili Wakili wa Serikali Nasorro Katuga 

Wakili huyo kwa niaba ya wenzake akaiomba Mahakama kutokana na sababu hiyo iahirishe shauri hilo hadi siku ya Jumatatu asubuhi, wakiamini kwamba shahidi wanayemtegea huenda akawa amepona na ikishindikana wako tayari kumleta shahidi mwingine kati ya mashahid wao 24 wanaotegemea kuwaleta mahakamani hapo.

Hata hivyo jopo ya mawakili wa Utetezi wakiongozwa na wakili Peter Kibatala, hakukubaliana na maombi ya mawakili wa Serikali kuhusu kuahirisha kesi hadi siku ya Jumatatu ili hali wana mashahidi wengi waliobaki ambao wanatakiwa kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo.

Kibatala ameiomba Mahakama kwamba kesi hiyo badala ya kupelekwa hadi Jumatatu, basi angalu kesho ndio iendele aidha kwa kuletwa shahidi mwingine au huenda shahidi huyo anaweza kuja mahakamani hapo.

Hoja hiyo pia ilikataliwa na mawakili wa Serikali wakisema hawana uhakika na mashahidi walionao kama wataweza kuja kutoa ushahidi hapo kesho hivyo si busara kuja mahakamani na hadithi ya kwamba wamekosa shahidi.

“Kuhusu kuairisha mpaka kesho na sitakukubali kwamba tuje kesho halafu tukaja na hadithi ya kukosa shahidi..ndiyo maana tukaomba tuahirishe mpaka Jumatatu ili kama shahidi hata kama anatakiwa kusafiri atakuwa amefika” amesema Wakili Nassoro Katuga.

Na kuongeza kusisitiza kuwa  “Sisi tunaona Kkuwa ni busara kuairisha mpaka kesho halafu tukaja na story, Mahakama yako itachoka kutusikiliza. Sisi tunaomba tupewe airisho mpaka Jumatatu.

Mara baada ya hoja hizo kuibuliwa kutoka pande zote mbili Jaji Joachim Tiganga amesema Mahakama imekua na shauku ya kumaliza shahuri hilo liishe haraka na mawakili wa pande zote wamekuwa wakiombwa kutokwamisha uendelezaji wa kesi hiyo kwa namna yeyote, lakini kutokana na maombi yaliyotolewa jana na shahidi na majibu juu ya afya yake hii  leo anavyoendelea ameonelea kwamba kesi hiyo iahirishwe hadi Jumatatu Februari 14,2022, ili kumpa muda shahidi wa kupumzika.

Hata hivyo Tiganga amewataka mawakili wa Serikali kuja na shahidi mwingine kadri itakavyowezekana

Lakaini shahidi huyu ni nani hasa? na ana umuhimu gani hasa kwenye kesi hii

Anaitwa Tumaini Sosthenes Swila, mwenye umri wa miaka 46, akitokea kabila la Mndali.

Dhehebu lake la dini ni mkrsto na ni mtumishi wa umma akiwa ni mkaguzi wa Polisi katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke.

Kazi yake kubwa katika kitengo chake ni Kuzuia Uhalifu, Kukamata watuhumiwa, na kupeleleza makosa ya jinai kazi amabayo ameifanya kwa takribani miaka 24 sasa.Taaluma yake ya upelelezi ameipata kupitia kozi mbalimbali pamoja na uzoefu kazini.

Shahidi ni muhimu katika kesi hii kwa sababu yeye ni mmoja ya askari waliohusika kumkata mshatakiwa wa kwanza katika kesi ugaidi Halfan Bwire, eneo la Temeke jijini Dar es salaam, lakini pia ndiye mtu anayedaiwa kupokea maelezo ya mshatkiwa wa pili na wa tatu ambapo washtakiwa hao walidai kuwa walichukuliwa maelezo wakiwa chini ya mateso.

Swila alianza kutoa ushahidi wake mbele ya mahakama mnamo Februari 4,2022 ambapo alianza kuhojiwa na mawakili wa serikali na kisha baada ya mawakili hao kumaliza maswali kwa shahidi upande wa utetezi ukapata nafasi ya kumuhoji shahidi huyo.

Alisema nini shahidi?

Katika kesi hiyo shahidi huyo wa 13 kati ya mashahidi 24 wanaotarajiwa kuletwa na upande wa Jamhuri wakati akihojiwa na mawakili wa Serikali aliiambia mahakama kua tarehe 27 Julai 2020 akiwa ofisi ndogo ya upelelezi Dar es Salaam, alipokea Jalada lenye kumbukumbu namba CD/IR/2097/2020 kosa kula njama za kutaka kufanya vitendo vya kigaidi. Jalada hilo lilikuwa limetolewa maelekezo na Afande Robert Boaz Kamishina wa Polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai nchini akitoa maelekezo kwa Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi pamoja na yeye akiwata waendelee na upelelezi wa kosa hilo la ugaidi linalomkabili Mbowe na wenzake watatu.

Mara baada ya kupokea jalada la kesi hiyo akaanza kazi aliyopangiwa lakini ilipofika Agosti 6,2021 majira ya saa 2 usiku alipokea simu kutoka kwa Afande Kingai ikimueleza kuwa tayari watuhumiwa wawili wamekamatwa.

Baada ya kupokea taarifa hizo, shahidi huyo yeye ameiambia mahakama kuwa aliendelea na kazi yake ya upelelezi kama alivyopangiwa  na kukiri kwamba alipokea maelezo ya watuhumiwa wawili ambao ni Mohamed Ling’wenya na Adam Kasekwa na kisha kuyahifadhi.

Katika upelelezi wake shahidi huyo amedia kuwa aligundua mawasiliano ya watuhumiwa hao ambayo kwa namna moja ama nyingine yalikuwa na viashiria vyaugaidi, na walikua wanatumia telegram kufanya mawasiliano yao

Hayo ni baadhi tu ya yaliyojiri katika kesi hiyo kwenye mahojiano ya wakili wa serikali na shahidi huyo wa 13, hata hivyo shahidi h pia aliiambia mahakama kwamba kesi hiyo haijafuguliwa kwa maslahi binafsi na hii baada ya kuulizwa maswali ya dodoso na wakili wa utetezi Peter Kibatala

Shahidi huyo bado hajamaliza kutoa ushahidi wake lakini huenda akamaliza ushahidi siku ya Jumatatu, 

Katika kesi hiyo ya msingi namba 16/2021, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili pesa kwa ajili vitendo vya kigaidi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire, Mohamed Ling’wenya na Adam Kasekwa maarufu kama Adamoo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted