Viongozi wa CCM wamjulia hali Profesa Jay Muhimbili

Waahidi kutoa ushirikiano katika kila hatua ya matibabu yake

0

Katibu Mkuu wa Chama Cha CCM, Daniel Chongolo na Katibu wa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka wamemtembelea aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Joseph Leonard Haule maarufu Profesa Jay aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu.

Chongolo amesema kuwa hali yake inaendelea kuimarika na wataendelea kutoa ushirikiano wa kila aina kuhakikisha matibabu yake yanaendelea vyema huku Watanzania wakiendelea kumuombea.

“Tumemuona ndugu yetu (Prof Jay) hali yake inazidi kuimarika, tumshukuru Mungu lakini niwashukuru madaktari kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kumhudumia lakini kwa Niaba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan niwahakikishie tutaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano katika kuhakikisha matibabu yanaendelea vyema huku tukiendelea kumuombea apone haraka” amesema Chongolo.

Profesa Jay ni mwanamuzi nguli wa nyimbo za miondoko ya kizazi kipya ambaye ameingia katika gemu la muziki zaidi ya miaka 10.

Kwa wengine humuita mwalimu wa muziki kutokana na ukongwe wake katika tasnia hiyo, licha ya kuingia kwenye siasa lakini karia yake ya muziki bado imeendelea kuishi ndani ya damu yake.

Msanii hiuyu amelazwa hospitali kwa takribani mwezi sasa akipata matibabu na ndani ya kipindi chote hicho amepita katika hospitali tatu ikiwemo, hospitali ya Lugalo na Muhimbili ambako ndipo sasa anakoendelea kupatiwa matibabu chini ya uangalizi maalum.

Hadi sasa bado familia yake haijawekwa wazi ni kitu gani kinamsumbua Profesa Jay, lakini kadri siku zinazovyoendelea huenda mashabiki wa msanii huyo watajua nini kilikua kikimsumbua.

Jana, katika mitandao ya kijamii lilisambaa tangazo likiomba kuchangia matibabu ya msanii huyo ambapo pia mke wa Profesa Jay, Grace Mgonjo alithibitisha kuwa wameruhusu michango hiyo baada ya kuona watu wengi wanania ya kuchangia matibabu ya Jay na si kwamba familia ilishindwa kumuhudumia.

Grace alisema kwamba matibabu ya Profesa Jay kwa wiki moja yanagharimu hadi kiasi cha shilingi milioni nne lakini pia hubadilika badilika kulingana na mwenendo wa matibabu hasa katika vipimo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted