Atelekeza gari lenye madini ya dhahabu yenye thamani ya zaidi milioni 140.

Ni baada ya polisi kumshtukia kuwa anayasafirsha kinyume cha sheria, kwa kukwepa kodi

0

Jeshi la Polisi Mkoani  Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa Madini Wilaya ya Chunya, limefanikiwa kukamata madini aina ya dhahabu yenye thamani ya shilingi milioni 147,694,961.83/=, yaliyokuwa yakisafirishwa kinyume na utaratibu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urich Matei, amesema mnamo tarehe 09.02.2022 majira ya saa 19:30 usiku huko katika kizuizi cha Polisi Chalangwa kilichopo Kata ya Chalangwa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Askari Polisi kwa kushirikiana na Maafisa Madini Wilaya ya Chunya walikamata Gari lenye namba T.948 DTM aina ya Toyota Crown iliyokuwa ikiendeshwa na mtu aliyefahamika kwa jina Baraka Singu, ali maarufu kama  NYODA, ambaye baada ya kusimamishwa kwenye kizuizi hicho alikimbia na kutelekeza gari hiyo.

Kamanda Mtei amesema katika upekuzi uliofanywa kwenye Gari hiyo vilikutwa vipande 36 vya madini aina ya dhahabu vyenye uzito wa gramu 1367.07 vyenye thamani ya shilingi 147,694,961.83/= na fedha taslimu shilingi 504,600/=. 

Amesema mtu huyu alikuwa na lengo la kukwepa kodi na tozo za serikali, hivyo Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa kwa hatua zaidi za kisheria. 

Aidha ametoa rai kwa wafanyabiashara kutambua kuwa mkono wa serikali ni mrefu hivyo ni vyema kufanya biashara halali kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo ili kuepuka kukinzana na sheria.

Katika hatua nyingine Jeshi hilo linamshikilia bwana Felix Ulimwengu(42), ambaye ni Mfanyabiashara na Mkazi wa Madale Jijini Dar es Salaam, kwa kosa la kusafirisha madini bila ya kuwa na kibali.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 08.02.2022 majira ya saa 14:45 mchana huko kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Songwe kilichopo Wilaya na Mkoa wa Mbeya,  wakati wa ukaguzi wa abiria waliokuwa wanasafiri kwa ndege ya kampuni ya ATCL kuelekea Dar es Salaam,  na kukutwa na madini aina ya Dhahabu kwenye Wallet yake yenye uzito wa Gramu 36 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne bila kuwa na kibali.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted