Matumizi ya P2 yanavyochochea mzunguko wa hedhi kwa mwanamke kuvurugika

Wataalam wanasema madhara mengine ya utumiaji wa P2 ni damu ya hedhi kwa mwanamke kuwa nzito kupita kiasi.

0

P2 ni neno la kifupi linalotambuliwa sana na watu hasa majumbani, lakini kitaalam linajulikana kama Postinor-2.

Kwa mujibu wa wataalaam hii ni dawa inayotumika kwa dharula tu, dawa ambayo mara nyingi hutumiwa kwa ajili ya kuzuia mimba.Wataalam wanashauri kwamba vidonge vya P2 havitakiwi kutumika kama njia ya mara kwa mara kuzuia mimba.

Vidonge vya p2 vinatakiwa kutumika tu endapo njia zingine za kuzuia mimba zimefeli. Kwa mfano kondomu kupasuka katikati ya tendo au umefanya tendo na kusahau kuvaa kinga na upo kwenye siku za hatari.

Vidonge hivi vinafanya kazi kwa kuzuia yai kupevuka wakati wa mzunguko wa hedhi. Pia vinafanya uteute wa ukeni kuwa mzito sana na kufanya mbegu kushindwa kuogelea kwenda kwenye yai. 

Kazi ya Vidonge vya P2.

Vidonge vya P2 vinazuia kushika mimba endapo vitatumika ndani ya masaa 72 baada ya kufanya tendo bila kinga. Inakadiriwa kwamba P2 ina ufanisi karibu asilimia 85 kuzuia mimba. 

Endapo vidonge vitatumika ndani ya masaa 24 baada ya kufanya tendo, ufanisi unaongezeka zaidi ya asilimia 95, lakini makali yake katika kufanya kazi mwilini hupungua kadiri masaa yanavyosogea

Kutumia vidonge vya P2 haina maana kwamba unaepuka magonjwa za zinaa kama vile Ukimwi, Kisonono, Chlamydia na mengineyo.

Vilelvile vidonge hivi havitumiki kutoa mimba, na hii ni baada ya watu wengi kutokua na elimu navyo na wasiofata ushauri wa wataalam kuamini kwamba P2 inatoa mimba.

Hata hivyo wataalam wanaonywa kwamba dawa hii inaweza isifanye kazi vizuri kwa baadhi ya wanawake hasa wenye uzito mkubwa mfano uzito zaidi ya kilo 74, na kama upo kwenye dozi ingine ya dawa, kabla ya kutumia P2 zungumza na daktari wako aone kama inakufaa kulingana na afya yako.

Ni yapi Madhara ya Matumizi ya P2

Dalili kama kichefuchefu, kutapika, maumivu ya tumbo, kuchoka sana, mabadiliko ya uteute ukeni, matiti kulainika, kuharisha au maumivu ya kichwa vinaweza kutokea baada ya kumeza P2.

Madhara mengine ni damu ya hedhi kuwa nzito kupita kiasi, kukosa kabisa hedhi na kupata maumivu makali ya kiuno.

Dawa hii inashauriwa na wataalamu wa afya kuwa itumike si zaidi ya mara 3 kwa mwaka kwani baadhi ya tafiti zimeonesha kuwa matumizi ya mara kwa mara ya dawa hizi yanaweza kupeleka mtu kupata saratani, kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi kutokana na kuvurugika kwa viwango vya homoni (vichocheo) na kuathiri vitu vingine vinavyotegemea vichocheo hivyo.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted