Vijana 2400 huambukizwa VVU kila mwezi

Maambukizi hayo ni sawa na vijana 28,800 wanaombukizwa VVU kwa mwaka.

0

Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI imeeleza kwamba vijana 80 huambukizwa Virusi vya UKIMWI kwa siku, kwa mwezi ni vijana 2400, sawa na maambukizi 28,800 kwa mwaka.

Hayo yamesemwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Fatma Tawfiq, wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa kipindi cha kati ya Januari mwaka 2021 hadio Februari mwaka 2022.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, wanachangia maambukizi kwa asilimia 40 ya maambukizi yote kitaifa, ambapo kiwango cha maambukizi kwa wasichana asilimia 2.1 na wavulana ni asilimia 0.6.

Sababu kubwa zinazochangia kuongezeka kwa maambukizi mapya kwa wasichana rika balehe ni kuanza ngono wakiwa na umri chini ya miaka 15 na wavulana asilimia 14.3 hufanya ngono na watu wasio rasmi.

Ili kukabiliana na janga hilo, Kamati imeishauri Serikali kuendelea kushirikiana na wadau, wazazi na walezi kutoa mafunzo ya malezi bora ya afya ya uzazi kwa vijana walioko shuleni na nje ya shule na hatua za mabadiliko ya tabia.

Katika hatua nyingine Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi imebaini ongezeko la matumizi ya vidonge vya kuzuia mimba (P2) kwa baadhi ya wasichana hasa wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24, jambo ambalo ni hatarishi kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

“Licha ya kuwa na lengo la kuzuia mimba, matumizi ya vidonge hivi ambavyo vimekuwa vikiuzwa kwa bei ya chini yamekuwa yakichochea maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,”amesema.

Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, baadhi ya wasichana wamekuwa wakiogopa zaidi mimba kuliko maambukizi ya VVU na hivyo wamekuwa wakitumia vidonge vya P2 kama njia mbadala ya kuzuia mimba na kuacha kutumia kondomu ambazo zingewakinga dhidi ya maambukizi ya VVU na magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa.

Amesema ili kukabiliana na tabia hiyo hatarishi, kamati inashauri kwamba wakati wa mauzo ya dawa za kuzuia mimba (P2) ni vizuri zikauzwa pamoja na kondomu kwa lazima ili kuwawezesha wasichana kuwa na tabia ya kutumia kondomu hizo bila ya kunyanyapaliwa.

Amesema uzoefu unaonyesha iwapo watakuwa na hizo kondomu basi wasichana wengi watazitumia ili kupunguza maudhi na madhara ya dawa za kuzuia mimba.

“Dawa hizi huharibu mzunguko wa hedhi na mfumo wa hormone za wasichana. Mara nyingi wasichana wakitaka wavulana watumie kondomu huwa wanapata tatizo la upatikanaji wake kwa kuwa maduka ya dawa yenye kuuza kondomu yanakuwa yamefungwa wakati wa usiku,”amesema.

“Ununuaji wa kondomu na dawa ya P2 kwa pamoja utasaidia kupunguza unyanyapaa miongoni mwa vijana na kusaidia kufanya utafiti wa maambukizi ya VVU kwa wasichana,”amesema.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted