Mbowe na wenzake wanyimwa chakula miezi 5 sasa

Wamedai kuwa wanapohudhuria mahakamani wakitoka kurudi mahabusu wanakuta chakula kimeshaliwa na magereza.

0

Mshtakiwa wa nne katika kesi ya Ugaidi na Uhujumu Uchumi, Freeman Mbowe, ametoa malalamiko kwa Mahakama kuwa yeye na washtakiwa wenzake kwenye kesi hiyo wanakosa haki ya kupata chakula kwa muda wa miezi mitano sasa.

Mbowe ameyasema hayo hii leo wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani hapo kwa usikilizwaji wa shahidi wa 13, ambapo ameeleza kuwa awali waliambia kuwa kama chakula wachuke kutoka jela waje nacho mahakamani lakini wakitoka mahakamani hapo wanakuta magereza wameshakula chakula hicho

“Mheshimiwa Jaji naomba kuleta Kwenye Mahakama yako kuwa tumekosa haki ya kula chakula mchana kwa Miezi 5, Wakati nyie Mna’ break kwenda kula sisi hatupati chakula wala maji kwa miezi Yote 5”- amesema Mbowe na kuongeza kuwa 

“Pale mwanzo tuliambiwa kuwa kama chakula tuchukue Kutoka Jela, tutoke nacho Jela tuje nacho Mahakamani, tkitoka hapa tunakutana Magereza Wameshakula tunakwe ndakulala na njaa siku zote.. Hawa vijana wanakonda kila Siku hata kusikiliza kesi ni geresha.. Ni hayo tu..”

Hoja ya Mbowe ikazua mshangao na sintofahamu ndani ya chumba cha Mahakama kiasi ambacho Jaji aneyeendesha kesi hiyo Jaji Joachim Tiganga, amewauliza mawakili wa utetezi kwamba “sasa nyie Kibatala mnatoa uwakilishi gani hapa Mahakamani kama wateja wenu hawali miezi mitano?”

Wakili Peter Kibatala kwa niaba ya mawakili wenzake amesema kuwa suala hilo walishalifikisha katika uongozi wa magereza na maamuzi yaliyotolewa ndio kama yalisemwa na mteja wake.

“Sisi tulifkisha kwa Officer wa Magereza, Suluhu aliyotoa ndiyo hiyo Asubuhi Watoke na Chakula Kutoka Jela Kitu ambacho tulibishana na hatukufikia Muafaka kwa sababu haiwezekani.. Nafikiri hata Msajili Wa Mahakama analijua hilo, sutaki kumsemea..” amesema wakili Peter Kibatala.

Hoja ya Kibatala ikamuinua wakili wa Serikali Robert Kidando ambaye ameona kuna haja ya kulizungumzia suala hilo kwa dharura na mawakili wengine pembeni.

Suala hilo likaungwa mkono na pande zote mbili, hali iliyomlazimu Jaji kuahirisha kwa muda kesi hiyo na kwenda kuzungumza na mawakili wa pande zote mbili pembeni. Hata hivyo muda mchache baadae Mbowe alikuja kuitwa na Jaji ili nae akawe miongoni mwa walioshuhudia maongezi hayo, juu ya kutafuta suluhu ya jambo hilo.

Mahakama iliporejea Jaji Joachim Tiganga akasema kuwa maamuzi yaliyotolewa ni kwamba wametafutwa wahusika kuelezwa jambo hilo, hivyo kwa hivyo wanasubiri uamuzi wao.

“Mshtakiwa Namba Nne aliibua Hoja ambayo tumekutana Mahakamani na Kuwatafuta Wahusika, Na tumemshirikisha yeye Mwenyewe Katika Mchakato Wa Kufikia Maamuzi, Kama una jambo la Kusema Mshtakiwa Wa Nne Karibu kabla ya Kusema Uamuzi..” amesema Jaji Tiganga

Hata hivyo Mbowe ameshukuru kwa hatua hiyo japo amedai kuwa ilikua nje ya utaratibu kwa kutowashirikisha mawakili wake kutokana na kwamba alitaka jambo hilo lishughulikiwe haraka.

“Mheshimiwa Jaji kwanza nashukuru kwa kunisikiliza pamoja ni nje ya utaratibu, sikuwashirikisha mawakili kutokana na kutaka lishughulikiwe kwa haraka nashukuru sana..Na kilichoendelea kwa Mahakama Kuu nimeshirikishwa kwa hatua zote.” amesema Mbowe na kuongeza kuwa

“Pamoja na kwamba tuna njaa ila nguvu za kuendelea kusikiliza kesi bado tunayo, kwa kuwa bado jambo litahusisha na idara zingine linaweza lisiishe leo. Kwa hiyo napenda tuendelee na shauri wakati tunasubiria maamuzi”

Mara baada ya majadiliano na maaumuzi kupatikana kesi hiyo hivi sasa inaendele kwa shahidi kuulizwa maswali ya dodoso kutoka upande wa mawakili wa Serikali.

Shahidi huyo ni 13 kutoka upande wa Jamhuri ambaye ni Inspekta Tumaini Swila alianza kutoa ushahidi Februari 2, mwaka huu kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando hadi Februari 9 alipoumwa ghafla wakati akihojiwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala.

Shahidi huyo aliugua ghafla akiwa kizimbani mwishoni mwa wiki, baada ya kuulizwa maswali na wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala.

Februari 9, mwaka huu, kesi iliahirishwa hadi Februari 10, kwamba shahidi alitakiwa kufika mahakamani kuendelea na ushahidi lakini hakutokea kwa madai alishauriwa na daktari apumzike.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, alidai shahidi hakuweza kufika mahakamani kuendelea na ushahidi, alishauriwa na daktari apumzike, hivyo hawataweza kuendelea kinyume na ushauri wa daktari.

Wakili Katuga aliomba kuahirisha kesi hadi leo kama shahidi atakuwa hajapona wanaweza kutafuta shahidi mwingine.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Freeman Mbowe, Adamu Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Halfani Bwire ambao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwamo kula njama kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei Mosi na Agosti 5, mwaka 2020.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted