Dk Mwele kuzikwa Februari 21

Baada ya mwili huo kuagwa Mvumi, utapumzishwa katika makazi yake ya milele.

0
Aliyekuwa Mkurugenzi wa WHO anayeshughulikia magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTD), marehemu Dk. Mwele  Malecela

Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa WHO anayeshughulikia magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTD), marehemu Dk. Mwele  Malecela(58), unatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam nchini Tanzania, usiku wa  Februari 18 ukitokea Geneva, Uswisi alipofikwa na mauti Februari 10,2022

Samwel Malecella ambaye ni msemaji wa familia ya waziri mkuu mstaafu, John Malecela,  amesema baada ya kuupokea mwili usiku wa Ijumaa, utapelekwa moja kwa moja nyumbani kwa ajili ya maombolezo

Amsema mwili huo utawasili kwa Ndege ya Shirika la KLM ukitokea Geneva nchini Uswisi ambapo mazishi yake yatafanyika Mvumi, mkoani Dodoma 21 Februari 2022.

“Siku ya Jumamosi asubuhi tutafanya sala fupi hapa nyumbani, ambapo familia watapata nafasi ya kumuaga ndugu yetu,” amesema Samweli ambaye ni mdogo wa Dk Mwele

Msemaji huyo wa familia amesema siku ya Jumamosi kuanzia saa 3.00 asubuhi, misa ya kumsindikiza Dk. Mwele, itafanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Alban.

Kisha majira ya saa 5.00 asubuhi, mwili wake utafikishwa kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutolewa heshima za mwisho kwa watu mbalimbali.

Aidha amesema, kutakuwa na  salamu mbalimbali kutoka kwenye makampuni, Serikali na watu binafsi watakaoweza kuja kutoa salamu zao za rambirambi.

Samweli amesema, baada ya zoezi hilo kukamilika kwenye Viwanja vya Karimjee, mwili utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kwa ajili ya safari kuelekea jijini Dodoma.

“Dodoma tunategemea kuwepo pale kuanzia saa 12.00 hadi saa 1.00 jioni, baada ya kupokelewa Uwanja wa Ndege wa Dodoma, tutaelekea moja kwa moja Hospitali ya Benjamini Mkapa, ambako tutampumzisha kwa siku hiyo ya Jumamosi,” amesema Samuel.

Mdogo wa huyo wa marehemu Dk. Mwele, amesema siku ya Jumapili mwili huo utafikishwa nyumbani kwao maeneo ya Kilimani majira ya saa 4.00 asubuhi, ambapo wananchi wataitumia siku hiyo kutoa heshima zao za mwisho.

Amesema, kesho yake Jumatatu ya tarehe 21 Februari 2022, itafanyika misa takatifu kwenye Kanisa la Anglican Dodoma Cathedral, kisha mwili utapelekwa Kata ya Mvumi, kwenda kutolewa heshima za mwisho kwa watu wa wilaya ya Chamwino.

Baada ya mwili huo kuagwa Mvumi, utapumzishwa katika makazi yake ya milele.

Dk. Mwele aliyekuwa mtoto wa Malecela, alijiunga na shirika afya duniani mwishoni mwa 2016.

 Aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR), ambapo uteuzi wake ulitenguliwa Desemba 2016 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.

Hadi umauti unamfika, alikuwa anasimamia miradi ya kupunguza magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele ya WHO, jukumu alilolishika kuanzia Oktoba 2018.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted