Waliomuua mtumishi wa Kanisa wapandishwa kizimbani

Wanadaiwa kumuua mtumishi huyo wa kanisa katoliki Makambako Nickson Myamba (46) kwa kumpiga na chuma na kumkata kwa panga vipande vipande

0
Daniel Mwilango(42) na Nickson Nyamideko(23) wanaodaiwa kufanya mauaji ya mtumishi huyo wa kanisa Februari 7,2022 mjini Makambako.

Watuhumiwa wa mauaji ya mtumishi wa kanisa katoliki Makambako Nickson Myamba (46)  wamefikishwa hapo jana katika mahakama ya hakimu mkazi Njombe.

Watuhumiwa hao ni Daniel Mwilango(42) na Nickson Nyamideko(23) wanaodaiwa kufanya mauaji ya mtumishi huyo wa kanisa Februari 7,2022 mjini Makambako.

Hakimu mkazi Mfawidhi Wilaya ya Njombe Matilda Kayombo akitaja shauri namba 5 la mwaka 2022 kuwa ni la mauaji yaliyotokea Makambako mkoani Njombe, alisema marehemu alikuwa katibu wa Halmashauri ya Walei Kanisa la Romani Katoliki Kigango cha Parokia ya Makambako mjini Njombe.

Wakili wa Serikali Magdalena Kisoka akisaidiwa na Paul Ngonyani walisema kosa wanalokabiliwa nalo ni Kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu Sura ya 16 ya sheria ya makosa ya jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Aidha hakimu Matilda Kayombo amepanga tarehe ya kusikilizwa shauri hilo ambapo itakuwa tarehe 28 Februari 2022 kutokana na kutokamilika kwa upelelezi wa shauri hilo.

Hata hivyo watuhumiwa hao wamerejeshwa rumande kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Watuhumiwa hao wawili Nickson Nyamwideko na Daniel Mwilango wanashikiliwa kwa tuhuma za kumpiga na chuma na kumkata kwa panga vipande vipande na kusababisha kifo cha Nickson Myamba kilichotokea mtaa wa Mangula Mjini Makambako mkoani Njombe.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted