Kenya yafuta kesi ya ufisadi dhidi ya kinara wa soka Nick Mwendwa 

Mwendwa alikamatwa Novemba baada ya serikali ya Kenya kuvunja Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na kuunda kamati ya muda ya kusimamia soka kwa madai ya ubadhirifu wa...

0

Mahakama ya Kenya leo imetupilia mbali mashtaka yote ya ufisadi dhidi ya kinara wa soka aliyesimamishwa kazi Nick Mwendwa baada ya waendesha mashtaka kushindwa kutoa ushahidi wowote dhidi yake.

Mwendwa alikamatwa Novemba baada ya serikali ya Kenya kuvunja Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na kuunda kamati ya muda ya kusimamia soka kwa madai ya ubadhirifu wa kifedha wakati wa uongozi wake.

Alishtakiwa kwa ubadhirifu wa shilingi milioni 38 (dola 337,000) alizopokea kutoka kwa serikali na wafadhili wengine pamoja na njama ya kulaghai FKF takriban $254,000.

Mwendwa, 43, alikuwa amekanusha madai yote dhidi yake.

Hakimu mkuu wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi Nairobi Eunice Nyuttu leo alifuta kesi hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kukosa tena kutoa mashahidi au ushahidi wowote.

“Ninamwachilia Mwendwa chini ya kifungu cha 87 (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPC) kwa kushindwa na DPP kutoa ushahidi mbele ya mahakama hii,” Nyuttu alisema.

Kufuatia kutimuliwa kwa Mwendwa na kusambaratishwa kwa FKF, Kenya ilisimamishwa na shirikisho la soka duniani FIFA mwezi Februari kutokana na kuingiliwa na serikali katika uendeshaji wa mchezo huo.

Kenya iliondolewa katika mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 yaliyoanza Juni, na haiwezi kuandaa au kucheza mechi zozote za kimataifa chini ya marufuku ya FIFA.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted