Waziri wa Afya nchini Tanzania asema hakuna mgonjwa mpya wa Mgunda

Amesema wagonjwa 17 waliokuwa wamelazwa kwenye kituo cha afya cha Ndekenyera tayari wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao.

0

Waziri  wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa Mgunda uliopo nchini humo unatibika na kwamba toka Julai 18, 2022 hadi asubuhi ya leo Julai 29. 2022, hakuna mgonjwa mpya.

Akizungumza jijiji Dar es Salaam leo,Waziri Ummy amesema idadi ya Wagonjwa wa homa ya Mgunda waliothibitishwa ni 20 na  kati yao watatu wamefariki.

Amesema habari njema ni kuwa “Ugonjwa huu unatibika kwa kutumia dawa antibiotiki”

Amesema wagonjwa 17 waliokuwa wamelazwa kwenye kituo cha afya cha Ndekenyera tayari wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao.

“Ugonjwa huu upo nchini na  ulibainika Ruangwa mkoani Lindi toka tarehe 18 hadi leo 29, habari njema ni kuwa ugonjwa huu unatibika, na si mara ya kwanza kuwepo nchini, mwaka 2014 ulibainika kuwepo Kigoma katika halmashauri ya Buhigu.” Amesema Ummy

Amesema “Habari nyingine njema ni kuwa ugonjwa huu hauambukizi kama ilivyo Covid 19 au Ebola, watu ambao waliambatana na wagonjwa wa Mgunda hawajapata maambukizi,”

Aidha, amewasisitiza wananchi kutokuwa na hofu kwa kuwa ugonjwa huo umedhibitiwa, na kwamba Serikali ina uwezo wa kuendelea kuchunguza, kutibu na imeweka mikakati ya kuudhibiti.

Aidha, Wizara ya Afya imeendelea kuwakumbusha wananchi kuendelea kuchukua tahadhari stahiki za kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuepuka kutumia maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama, kunywa maji safi na salama pamoja na wagonjwa wanaohisi dalili zilizotajwa na Wizara kufika hospitali kwa ajili ya uchunguzi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted