Makali Ya Ukame Yawahamisha Wakaazi Wa Wajir Hadi Tana River Nchini Kenya

afugaji kutoka kaunti ya Mandera na Wajir wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 100 hadi kaunti jirani ya Tana River angalau kupooza makali ya njaa yanayoawaathiri na mifugo wao.

0


Ukame unaendelea kusakama wanadamu na mifugo eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya huku wakaazi sasa wakilazimika kuhama makwao kutafta maji na lishe ya mifugo.


Hali imekuwa mbaya zaidi kiasi cha wafugaji kutoka kaunti ya Mandera na Wajir wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 100 hadi kaunti jirani ya Tana River angalau kupooza makali ya njaa yanayoawaathiri na mifugo wao.


Wafugaji ambao wamepiga kambi katika wadi ya Sala kaunti ndogo ya Bura kaunti ya Tana River wameelezea huzuni yao kuhusu zimwi la ukame ambalo limeendelea kutishia maisha yao.


Farida Hassan ambaye ni mkaazi wa Mandera anasema kuwa kuhamahama kutokana na kiangazi kumewaacha bila makao huku wengi wa mifugo wao wakifariki.Wanakijiji wa wadi ya Sala hata hivyo waliwakaribisha na kuwasaidia kujenga vyumba vya kushikilia kwa muda kwa ajili ya familia zao.


“Wengi wa mifugo wetu walifariki tukiwa njiani hii ikilemaza kipato chetu cha chakula na fedha.tunaiomba serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kutusaidia kwani watoto wetu hawana uwezo wa kuenda shuleni kwani wanasakamwa na njaa”alisema.


Farida amewashukuru wanakijiji wa Hamaresa kwa kuwakaribisha na kuwapa makaazi licha ya kuwa wanapitia masaibu sawa na wao.Anasema kuwa watoto hawajafika shuleni tangu janga la ukame kuanza.


Muhamed Mude ambaye pia ni mfugaji amelaumu hali ya ukame wanaoshuhudia kuwa chanzo cha wao kukosa maji na lishe ambayo imepelekea wao kukumbwa na baa la njaa na kufariki kwa mifugo wao huku sasa wakilazimika kuhama makwao.


Mwakilishi wadi wa Sala,Mohamud Ali Barrow amewaomba viongozi waliochaguliwa kaunti ya Wajir kuwasaidia wakaazi waliowapigia kura huku akiyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile shirika la msalaba mwekundu kuwasaidia ili kuokoa maisha.


“Kilomita 14 ndio umbali kutoa Tana River hadi kijiji hiki na hii ndio umbali wa karibu zaidi ambao wakaazi wanaweza pata maji na hivyo basi hii inaonyesha jinsi maji ni changamoto kuu hapa.Ni sababu ndio imenifanya nimekuwa natuma malori ya kusafirisha maji”alisema mwakilishi wadi .


“Naiomba serikali ya kaunti ya Tana River kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa kusaidia kuleta suluhu na kusaidia haswa watoto kurejea shuleni .Tutashukuru zaidi tukipata chakula cha msaada.”aliongeza.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted