Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanasababisha vifo 33 kati ya vifo 100 ambavyo ni takriban vifo vinne katika kila vifo kumi vinavyotokea nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Novemba 9,2022 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasper Mmuya katika maadhimisho ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza (NCD) katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Amesema magonjwa yasiyo ya kuambukizwa nchini yanachochewa na tabia bwete watu wengi wakiwamo vijana kutoshughulisha miili huku wengi wakiwa hawafanyi mazoezi.
“Kuna tabia imejengeka miongoni mwa vijana, wakitoka kazini badala wajishughulishe na mazoezi au kujadili mambo ya maendeleo, wanaenda baa kunywa pombe kali na wengine wanatengeneza mchanganyiko wa pombe kali wanakunywa, wanajitengenezea bomu mwilini bila kujijua,” amesema Mmuya.
Aidha, amewataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kujua hali ya afya zako ikiwa ni pamoja na kuzingatia ulaji unaofaa wa vyakula.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk James Kiologwe amesema zaidi ya robo tatu ya wananchi hawajitambui kuwa wana magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kutaka elimu zaidi itolewe.
Amesema mwanamke mwenye magonjwa yasiyoambukiza yupo katika hatari zaidi ya kujifungua watoto wenye uzito pungufu na pia wapo kwenye hatari zaidi ya kurithisha vizazi vinne, cha kwanza, cha pili, cha tatu na cha nne.
Katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu: ‘Badili Mtindo wa Maisha Boresha Afya.’ Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambaye ni Mratibu Wadau Sekta ya Afya, Leticia Rweyemamu, amesema asilimia 74 ya vifo vinavyotokea duniani vinasabishwa na magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa mujibu wa Rweyemamu, mwaka 2012 kulikuwa na vifo milioni 157 kati ya hivyo, milioni 41 vilichangiwa na magonjwa yasiyoambukiza. Tangu mwaka 2016 takwimu hizo zimekuwa zikiongezeka na kufikia asilimia 74.
“Kila mwananchi akijitambua, tutafika lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa hayo ambayo ni mzigo mkubwa kwa familia na taifa kwa kuwa licha ya kuwaathiri wagonjwa, huchangia ongezeko la umaskini,”amesema.
Amesema mtindo usiofaa wa maisha ukiwamo ulaji mbovu ni miongoni mwa mambo yanayoongeza kasi ya magonjwa hayo ambayo ni pamoja na kisukari, presha na moyo