Mchakato wa usikilizwaji wa kesi inavyohusiana na kukamatwa kwa mwanahabari Erick Kabendera, aliyoifungua mwanahabari huyo dhidi ya kampuni ya huduma za Mawasiliano Kwa simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Ltd unaanza leo.
Kabendera ambaye alikuwa amejikita katika uandishi wa Habari za uchunguzi akifanyia kazi kampuni tofauti nje na ndani ya Tanzania
Katika kesi hiyo Kabendera anaoimba mahakama hiyo iiamuru kampuni hiyo imlipe fidia ya Dola za Marekani 10 milioni ambazo ni sawa na shilingi bilioni 28, akiituhumu kuwa ndio iliyofanikishwa kukamatwa kwake na askari Polisi, tukio analoliita kutekwa, na kisha kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi, mwaka 2019.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa na Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi na pande zote zimeitwa kufika mahakamani hapo leo Julai 9, 2024.
Kulingana na hati ya wito wa mahakama kwa watajwa toka pande zote wanapaswa kufika mahakamani, kesi hiyo namba 12799/2024 imepangwa kutajwa asubuhi hii, huku ikiitaka kampuni hiyo kufika bila kukosa na kuwasilisha nyaraka zake ambazo inatarajia kuzitumia katika utetezi wake.
Katika kesi hiyo Kabendera anadai kuwa kutokana na matukio hayo amepata madhara ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi, ya kijamii, maumivu ya kiakili na kimaono, hasara ya kutokufurahia maisha hasara ya maendeleo binafsi na hadhi yake katika jamii na kutokuaminiwa kitaaluma.
Hivyo anaitaka kampuni hiyo imlipe kiasi hicho cha pesa, kama fidia ya hasara halisi na riba kwa kiwango cha mahakama kuanzia tarehe ya hukumu mpaka kumaliza malipo yote.
Pia anataka alipwe fidia ya hasara ya jumla kadri mahakama itakavyotathmini, gharama za kesi na nafuu nyingine kadri mahakama itakavyona inafaa.