Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama cha ACT- Wazalendo, Abdul Nondo alitelekezwa jana usiku katika fukwe za Coco jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ya Polisi iliyotolewa leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 na msemaji wake, David Misime imeeleza baada ya kutelekezwa katika fukwe hizo, aliomba msaada wa bodaboda kumfikisha katika ofisi za chama chake Magomeni, Dar es Salaam.
“Desemba mosi, 2024 majira kama saa nne na nusu usiku Abdul Omary Nondo ambaye tulikuwa tunamtafuta kwa kushirikiana na watu mbalimbali, wakiwepo viongozi wake wa chama cha ACT Wazalendo baada ya kukamatwa na kuchukuliwa kwa nguvu pale kituo cha mabasi cha Magufuli ameeleza alitelekezwa maeneo ya fukwe za Coco (Coco Beach) Kinondoni, Jijini Dar es Salaam na watu asiowafahamu.
“Baada ya kutelekezwa alisimamisha bodaboda na kumwelekeza amfikishe katika ofisi za chama chake zilizopo Magomeni, Jijini Dar es Salaam na walifika muda wa saa tano usiku,” imeeleza tarifa hiyo na kuongeza kuwa alionana na viongozi wake na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
TUKIO LILIVYOKUA
Taarifa za kutekwa kwa Abdu Nondo zilisambaa jana katika mitandao ya kijamii ambapo baada ya kusambaa kwa taarifa hizo chama chake kiliwataka wanaomshikilia kumwachia haraka kwani kinajua mmiliki na lilikoegeshwa gari lililotumika kumteka.
Nondo anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana jana alfajiri kwenye Stendi ya Mabasi ya Magufuli, iliyoko Mbezi Loius, wilayani Ubungo, Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi lilisema linachunguza tukio hilo ili kubaini waliomchukua Nondo, wakitumia gari lenye rangi nyeupe aina ya Toyota Landcruizer.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi wa chama hicho, Mbarala Maharagende, Nondo alitekwa alfajiri ya jana na watu wasiojulikana, akitokea mkoani Kigoma alikokuwa sehemu ya viongozi wa kitaifa walioongoza kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mikoa ya magharibi mwa nchi.
Maharagande alidai Nondo aliwasili Stendi ya Mabasi ya Magufuli kwa usafiri wa basi la Saratoga lenye namba za usajili T 221 DKB.
“Mashuhuda wa tukio wamesema kuwa kulikuwa na purukushani katika utekaji wa Nondo iliyosababisha begi lake dogo la nguo na pingu iliyobebwa na mmoja wa watekaji kudondoka.
“Katibu Mwenezi Mkoa wa Dar es Salaam,Monalisa Ndala na Ofisa wa Harakati na Matukio Taifa, Wiston Mogha, waliofika mapema kituoni huko walitambua haraka kuwa aliyetekwa ni Abdul Nondo kwa sababu walizitambua nguo zake kwenye begi lililodondoka na notebook yake,” alisema Maharagande.
“Chama kinaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hili na kitatoa taarifa zaidi kwa umma. Katika hatua ya sasa tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Cammilius Wambura, kufuatilia haraka tukio hili na kuhakikisha Abdul Nondo anaachiwa huru mara moja,” aliongeza.
Hata hivyo, Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe, alimtaja kwa jina mmiliki wa gari hilo linalodaiwa kutumika katika utekaji huo.
“Tunataka Abdul Nondo aachiwe huru mara moja akiwa mzima wa afya. Tafadhali sana, gari inadaiwa ‘parking’ (maegesho) na tumejua kila mahala gari hiyo inaegeshwa, mwacheni Nondo haraka iwezekanavyo,” alisema.
Tukio hili linafanana na kutelekezwa na kuuawa kwa Ali Mohamed Kibao, kiongozi wa Chadema, chama kikuu cha upinzani, ambaye alidaiwa kupatikana akiwa amekufa baada ya kupigwa na kumwagiwa tindikali mnamo mwezi Septemba.
Uchaguzi huu wa mitaa ulikuwa jaribio la kwanza la uchaguzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake, Rais John Magufuli, mwaka 2021.
Awali, Rais Samia alikubalika kwa kupunguza vizuizi vilivyowekwa na Magufuli kwa upinzani na vyombo vya habari nchini Tanzania yenye watu takriban milioni 67.
Hata hivyo, makundi ya kutetea haki za binadamu na serikali za Magharibi zimekiri kile wanachosema ni kurudi kwa ukandamizaji, huku wakiwaona viongozi wa Chadema wakikamatwa na pia kutekwa na kuuliwa kwa viongozi wa upinzani.