Kampeni za urais Tanzania kuanza rasmi huku mgombea wa ACT Wazalendo akizuiwa kugombea

Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania zimeanza rasmi leo Alhamisi, huku jumla ya wagombea 17 wakiidhinishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kushiriki kinyang’anyiro cha urais, kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.

Hata hivyo, uchaguzi umeanza kwa changamoto baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, ikidai ukiukaji wa taratibu za kisheria katika mchakato wa uteuzi wa chama. Uamuzi huo ulitangazwa Jumanne, siku moja kabla ya muda wa mwisho wa kurejesha fomu za uteuzi, na baadaye ukaidhinishwa na INEC.

Ofisi ya Msajili ilimwengua Mpina kufuatia pingamizi lililotolewa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala, ikibainisha kuwa Mpina alijiunga na ACT-Wazalendo mnamo Agosti 5, 2025 – baada ya muda wa kisheria wa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, ambao ulipaswa kuwa kabla ya Mei 25, 2025. Hali hiyo imesababisha chama hicho kushindwa kushiriki katika nafasi ya urais mwaka huu.

ACT-Wazalendo tayari imepanga kupinga uamuzi wa Msajili na Tume Mahakamani, ikisisitiza haki ya chama na mgombea wake katika mchakato wa kidemokrasia.

Ratiba ya kampeni za vyama vikuu

Kwa mujibu wa INEC, jumla ya vyama 18 vilivyosajiliwa vitashiriki uchaguzi huu, na wagombea 17 wa urais watashiriki kinyang’anyiro. 

Hali hiyo imefanya uchaguzi huu kuanza huku baadhi ya wagombea wakubwa wa upinzani kutoshiriki, wakidai mfumo wa uchaguzi wa sasa unakinufaisha chama tawala na hautoi usawa wa ushindani.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kuzindua rasmi kampeni zake leo Agosti 28, 2025 katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam. 

Mwenyekiti wa CCM na mgombea urais, Dk. Samia Suluhu Hassan, atakuwa kiongozi wa uzinduzi huo, akifuatana na mgombea mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi. Uzinduzi huu utaashiria mwanzo rasmi wa kampeni za CCM kwa nafasi za urais, ubunge na udiwani.