, ,

Shahidi : Sioni ia ya Lissu Kuitishia Serikali Katika Hotuba

Wadh Kassim Avatar

Shahidi wa nne wa upande wa utetezi, Brenda Rupia, amesema haoni nia ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hotuba ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ambayo imekuwa sehemu ya msingi wa kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi huyo.

Shahidi : Sioni nia ya Lissu kuitishia Serikali katika hotuba

Brenda, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, amesema hayo leo wakati akiendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Mahakama Kuu, akiongozwa na Lissu katika hatua ya ushahidi wa utetezi.

Amesema alikuwepo katika mkutano ambao Lissu alikuwa mzungumzaji mkuu na kwamba mkutano huo ulichukua takribani saa mbili hadi mbili na nusu, huku Lissu akizungumza kwa muda mrefu zaidi kuliko wazungumzaji wengine.

Kwa mujibu wa Brenda, sehemu ya maneno yaliyomo katika hati ya mashtaka ambayo Lissu alimuuliza kuhusu maana yake, haikuchukua zaidi ya dakika mbili katika hotuba hiyo.

Brenda amedai kuwa katika maneno hayo hakuna yaliyotaja Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri, Naibu Waziri, Mkuu wa Mkoa au kiongozi mwingine wa Serikali.

Pia amesema hakusikia maneno yanayohusu jeshi, kuvunja sheria, kupiga watu, kukata vidole, kuchoma vituo vya mabasi au vituo vya kupigia kura, wala kuwaua askari polisi.

Alipoulizwa na Lissu iwapo mtu akisema maneno hayo yanaitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Brenda amejibu kuwa kwa mtazamo wake si kweli kwa sababu, amesema, maneno hayo hayaitishii Serikali.

Aidha, Brenda amesema kauli kama “tutazuia uchaguzi” au “tutavuruga uchaguzi” kwa ufahamu wake si kosa, huku akieleza kuwa neno “kukitukisha” au “kukininukisha” ni lugha ya mtaani (slang), si neno la kawaida la Kiswahili.Akitoa mtazamo wake kuhusu hotuba hiyo kwa ujumla, Brenda amesema haiashirii kosa lolote.

–Video ya Jambo TV-Katika ushahidi wake, Brenda amesema aliiona video ya mkutano huo kwenye mtandao wa Jambo TV na kwamba kwa kumbukumbu zake video hiyo ilikuwa na urefu wa kati ya saa mbili na nusu hadi tatu.

Hata hivyo, amesema maneno yaliyotajwa katika hati ya mashtaka hayakuwa ndiyo yaliyomo kwenye video yote.

Brenda pia amesema alikuwepo kwa kiwango kikubwa wakati mashahidi wa upande wa mashtaka walipokuwa wakitoa ushahidi mahakamani, lakini hajawahi kuiona video iliyowasilishwa au kuonyeshwa mahakamani ikiwa na maneno mafupi yaliyotajwa kwenye mashtaka.

Amesema zaidi ya maelezo ya mashahidi wa upande wa mashtaka, hakushuhudia ushahidi mwingine wowote kuhusu suala hilo.

–Brenda asimulia kukamatwa kwake Namanga-Katika sehemu nyingine ya ushahidi wake, Brenda ameeleza namna alivyokamatwa Julai 12, 2025 katika mpaka wa Namanga wakati akielekea Nairobi, Kenya, kabla ya kuendelea na safari ya kwenda Ujerumani kwa mafunzo ya mawasiliano.

Amesema alikuwa ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Chadema kwenda kwenye mafunzo hayo ya “Communication in Leadership”, lakini hakufanikiwa kuvuka mpaka baada ya kukamatwa.

Brenda amesema baada ya kukamatwa alisafirishwa kwa gari aina ya Probox kutoka Namanga kuelekea Longido, likiwa linaendeshwa kwa kasi ya zaidi ya kilomita 120 kwa saa, na kwamba watu waliokuwa wakimsafirisha hawakumweleza sababu ya kumpeleka kituo cha polisi Longido.

Amesema baadaye alisafirishwa hadi Arusha, ambako alikutana na Mkuu wa Polisi Mkoa (RPC) wa Arusha, kabla ya kukabidhiwa kwa watu wengine waliomsafirisha hadi Dar es Salaam kwa gari aina ya V8 lenye namba za usajili za Zanzibar.

Kwa mujibu wa Brenda, walifika Dar es Salaam majira ya saa 10 usiku na baadaye walifika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) ambako walikutana na George Bagemu, aliyemtaja kuwa Naibu ZCO.

Brenda amesema Bagemu alimwambia alikuwa akimsubiri na kwamba angemweka ndani kwa zaidi ya wiki mbili. Hata hivyo, amesema baadaye aliambiwa amekamatwa kutokana na taarifa kwa umma aliyotoa Julai 2, 2025 kuhusu madai ya njama za kumuwekea sumu Lissu akiwa gerezani.

Amesema simu yake na pasipoti yake vilikabidhiwa kwa Bagemu na kwamba hadi sasa hajarejeshewa vitu hivyo.

Baada ya hapo, Brenda amesema alipelekwa nyumbani kwake Basihaya ambako polisi walifanya upekuzi katika vyumba mbalimbali, kabla ya kurejeshwa Central na kuwekwa mahabusu.

Amesema alikaa kituoni hapo kwa siku nne huku mawakili wa Chadema wakifanya taratibu za kisheria, lakini hakuwahi kufikishwa mahakamani wala kushtakiwa hadi wakati anatoa ushahidi huo.

Akieleza maudhui ya hotuba ya Lissu kwa ujumla, Brenda amesema Mwenyekiti huyo alizungumzia matatizo yaliyotokea katika chaguzi zilizopita, sababu za nchi kuhitaji mabadiliko na umuhimu wa kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu msimamo wa Chadema wa “No Reforms, No Elections”.

Amesema pia kauli kuhusu uasi ilihusishwa na kundi la G55, ambalo alidai lilikuwa kundi la watu ndani ya chama waliokuwa wakitaka Chadema ishiriki uchaguzi.

Kwa mujibu wa Brenda, Lissu alikuwa akieleza sababu za chama kupinga uchaguzi ambao, kwa mtazamo wao, haukuwa wa haki.

Alipoulizwa kama katika hotuba hiyo yote aliona nia ya kuitishia Serikali, Brenda amejibu:“Sioni nia ya kuitishia Serikali katika hotuba yote ile.”Brenda: “Ni ngumu Lissu kuwa mhaini”Brenda amesema anamfahamu Lissu kwa takribani miaka 13 na amemtaja kama kiongozi anayepigania demokrasia na haki.

Amesema kutokana na namna anavyomfahamu Lissu, ikiwemo misimamo yake ya kisiasa na harakati zake za kutetea haki, kwake ni vigumu kumtaja kuwa mhaini wa nchi yake.

“Kwa maneno yangu yanaonyesha ni mtu mwenye mapenzi makubwa na nchi yake, ni ngumu kuwa mhaini,”amesema Brenda.

Our Correspondent Avatar