, , , , , ,

Heche atoa wito kwa Ruto kumsaidia kumpata Twaha Mwaipaya aliyeritopiwa kutekwa Kenya

Victor Wanaswa Avatar

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, ametoa wito kwa Rais wa Kenya, William Ruto, na serikali yake kusaidia kuhakikisha mwanaharakati wa haki za binadamu na mwanasiasa wa upinzani kutoka Tanzania, Twaha Mwaipaya, anapatikana akiwa hai na salama, baada ya kuripotiwa kutekwa nchini Kenya.

Katika andiko alilochapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Heche amesema wamejitahidi usiku kucha kuwasiliana na vyombo vinavyohusika nchini Kenya ili kupata taarifa kuhusu aliko Mwaipaya.

Mwaipaya ni mwanaharakati wa kisiasa ambaye ni mwanachama wa CHADEMA, akiwa amewahi kutumikia chama hicho kwa ngazi mbalimbali ikiwemo Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA).

Amekuwa akiishi uhamishoni nchini Kenya baada ya kuondoka Tanzania, huku taarifa za wanaharakati wa haki za binadamu zikihusisha kuondoka kwake na madai ya vitisho na vitendo vya ukatili nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Amnesty International Kenya, Mwaipaya aliripotiwa kutekwa Jumapili, Oktoba 25, 2026, majira ya saa nane mchana katika eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos, karibu na mji mkuu wa Nairobi.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake wakati watu wasiojulikana waliokuwa katika magari matatu, yakiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop, walipomchukua.

Amnesty International imezitaka mamlaka za Kenya kuchunguza tukio hilo kwa haraka, kubaini alipo na kuhakikisha usalama wake.

Heche amesema haamini kuwa serikali ya Kenya ina sababu ya kumteka Mwaipaya, lakini ameeleza wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa watu kuingia katika nchi nyingine na kumchukua mtu bila msaada au ushirikiano kutoka kwa watu wenye mamlaka nchini humo.

Amesisitiza kuwa iwapo itathibitika kuwa utekaji huo umefanyika ndani ya mipaka ya Kenya, tukio hilo litakuwa doa kwa serikali ya nchi hiyo, akibainisha kuwa mtu anayekimbilia nchini humo kutafuta hifadhi anapaswa kulindwa.

Katika andiko hilo, Heche pia amedai kuwa vitendo vya mauaji, utekaji na kunyamazisha watu wanaopinga maovu vimekuwa vikiendelea nchini Tanzania.

Amewataka Watanzania kutokubali hali hiyo kuendelea.

Heche amehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kuwa wanachokitaka ni Mwaipaya kupatikana akiwa hai na salama, huku wito ukiendelea kwa mamlaka za Kenya kuchukua hatua za haraka kubaini alipo.

Our Correspondent Avatar