Chama cha The Equitable Paty kinachoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna kimebadilishwa rasmi na kuwa Linda Mwananchi katika hafla iliyohudhuriwa na kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa DAP-Kenya Eugine Wamalwa.
Chama hicho kimezindua rasmi afisi katika mtaa wa Lovington Jijini Nairobi na kumtangaza Edwin Sifuna kama mwaniaji wao wa urais huku muungano wa upinzani ukiendelea kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.
Sifuna akizungumza katika hafla hiyo, alisema kuwa viongozi wa upinzani watashirikiana hadi tamati na kumtoa mgombea mmoja katika juhudi za kumbandua rasi Ruto mamlakani katika uchaguzi huo wa mwakani.
Sifuna, alimtangaza aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kuwa miongoni mwa viongozi wakuu watakaokuwa katika mstari wa mbele kwenye azma yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu.
Sifuna alisema vuguvugu hilo litafanya Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) Novemba 13 ili kuidhinisha orodha ya viongozi waliopendekezwa.
Alieleza matumaini kuwa kikosi hicho, kinachojumuisha viongozi wenye uzoefu na ari ya kisiasa, kitasaidia kutekeleza maono yake ya kisiasa.
Kulingana na orodha iliyopendekezwa, Sifuna kama kinara atasaidiwa na aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo pamoja na Mbunge wa Mavoko Patrick Makau.
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi amependekezwa kuwa mwenyekiti, huku Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu, akisaidiwa na Pauline Njoroge.
Mbunge wa Funyula Oundo Mudenyo atakuwa Naibu Katibu wa Masuala ya Uratibu, huku Seneta wa Kisii Richard Onyonka akiteuliwa kuwa Mweka Hazina wa Kitaifa na kusaidiwa na Abigael Gikonyo.
Aliyekuwa Mbunge wa Makadara Reuben Ndolo naye amependekezwa kuwa Naibu Mwenyekiti.
Kwa upande wake, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya atakuwa mwenyekiti wa bodi ya wadhamini na pia kuongoza kikosi cha kampeni za urais, akisaidiwa na Faith Odhiambo.
Hata hivyo, Sifuna alisisitiza kuwa orodha hiyo si ya mwisho, akisema bado kuna nafasi nyingi za uongozi zitakazojazwa baada ya mashauriano zaidi.
“Timu hii bado haijakamilika. Kuna nafasi nyingi sana ambazo bado zinahitaji kujazwa, na tutafanya mashauriano kabla ya kufanya uteuzi huo,” alisema Sifuna.
Aliongeza kuwa ndani ya mwezi mmoja ujao, vuguvugu hilo litafungua zaidi ya ofisi 40 za matawi katika maeneo mbalimbali nchini, akiwakosoa wale wanaotilia shaka uwezo wao wa kutekeleza mpango huo.
“Wale waliofikiri hatuwezi kufanikisha hili walifanya hivyo kwa sababu wao ni wavivu,” alisema.
Akizungumzia kujitenga kwao na ODM, Sifuna alisema kuwa wameondoka na misingi na mafanikio ya chama hicho, huku akiwashutumu baadhi ya waliosalia kwa kusaliti ndoto za aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga.
“Tuliondoka na msingi, madirisha na milango… tumewaachia mende na mchwa pekee waliokula ndoto ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga,” alisema Sifuna.







