Mashirika ya uajiri nchini Kenya yanakadiria hasara kubwa za kifedha huku maelfu ya Wakenya waliokuwa wameajiriwa nchini Saudi Arabia wakikumbwa na sintofahamu kufuatia kukatizwa kwa safari kutoka na na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola aina ya Bundibugyo.
Muungano wa Mawakala wa Ajira nchini (KAPEA) unasema mashirika hayo yametumia fedha nyingi kugharamia tiketi za ndege, mchakato wa kupata pasipoti, vipimo vya afya pamoja na maandalizi mengine ya kuwasafirisha waliokuwa wanatarajiwa kuelekea nchini humo.
Utata huo wa usafiri pia umewaathiri waajiri nchini Saudia Arabia pamoja na familia zilizokuwa zimekamilisha taratibu za viza, kuwahoji wanasaka ajira na kujiandaa kuwapokea wafanyikazi hao.
KAPEA sasa inaitaka serikali ya Kenya kuimarisha mazungumzo ya kidiplomasia na Saudi Arabia, ikisema hatua zilizopigwa katika kudhibiti mlipuko wa Ebola zinapaswa kuwezesha mazungumzo ya kurejesha safari za kawaida kati ya mataifa hayo mawili.
Muungano huo umesema serikali imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na Ebola, ikiwemo kuwafuatilia watu wote 135 waliotambuliwa kuwa walitangamana na wagonjwa, kuruhusu wagonjwa waliopona kurejea nyumbani na kuwaachilia hatua kwa hatua watu waliokamilisha kipindi cha karantini.
Pia umepongeza Wizara ya Afya, wahudumu wa afya na vikosi vya kukabiliana na mlipuko huo kwa juhudi zao za kudhibiti ugonjwa huo, huku ukitambua mchango wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC).
KAPEA imesema mazungumzo yanayoendelea kupitia Wizara ya Kazi na Ulinzi wa Jamii pamoja na Wizara ya Masuala ya Kigeni yanapaswa kuimarishwa ili kupata suluhisho linalozingatia maslahi ya mataifa yote mawili.
Chama hicho kimesisitiza kuwa kukatizwa kwa safari hizo hakujaathiri wafanyakazi na mashirika ya ajira ya Kenya pekee, bali pia familia na biashara nchini Saudi Arabia zinazotegemea wafanyakazi kutoka mataifa ya nje.
“Waajiri na familia nchini Saudi Arabia ambazo zimetumia muda na rasilimali kukamilisha taratibu za viza, kufanya mahojiano na wafanyakazi watarajiwa na kujiandaa kuwapokea pia zimeathirika,” kilisema chama hicho.
“Matumaini yao ya kuwapokea wafanyakazi na kuendeleza shughuli za nyumbani na biashara yanapaswa kuzingatiwa.”
Muungano huo aidha, umeelekeza macho yake katika mwezi mtukufu wa Ramadhani unaokaribia, ukisema ucheleweshaji wa safari unaweza kuwaathiri waajiri na familia zinazojitayarisha kwa kipindi hicho, pamoja na Wakenya wanaopanga kusafiri nchini Saudi Arabia kwa shughuli za kidini, kibiashara na kifamilia.
Kwa upande wa mashirika ya ajira, kukatizwa kwa safari kumeongeza mzigo wa kifedha kwa kampuni ambazo tayari zilikuwa zimetumia fedha nyingi kukamilisha taratibu za kuwaajiri na kuwasafirisha Wakenya kupata kazi nje ya nchi.
Maelfu ya wanaotafuta ajira pia wameachwa gizani kuhusu ni lini wataanza kazi walizokuwa wameajiriwa kufanya, huku baadhi yao wakikabiliwa na uwezekano wa kusubiri kwa muda zaidi licha ya kukamilisha hatua kadhaa za mchakato wa kuajiriwa.
KAPEA imeitaka serikali kuendelea na mashauriano na mamlaka za Saudi Arabia kupitia njia za kidiplomasia, ikisema makubaliano yatakayofikiwa yatasaidia kutatua changamoto zinazowakabili waajiri, ikisema makubaliano yatakayofikiwa yatasaidia kutatua changamoto zinazowakabili waajiri, mashirika ya ajira na Wakenya wanaotarajia kupata kazi nchini humo.
Chama hicho kimesisitiza kuwa hatua za kulinda afya ya umma zinapaswa kuendelea kutekelezwa huku serikali hizo mbili zikitafuta suluhisho la changamoto za usafiri.
“Kwa kushirikiana, kufanya mazungumzo na kuelewana, tunaweza kulinda afya ya umma huku tukihifadhi fursa za ajira na uhusiano wa muda mrefu unaowaunganisha wananchi wa Kenya na Saudi Arabia,” kilisema chama hicho.
Sekta ya kuwaajiri Wakenya kwa ajili ya kazi za ng’ambo ni muhimu katika kutoa fursa za ajira nje ya nchi, hususan katika mataifa ya Ghuba, ambako maelfu ya Wakenya hutafuta kazi za nyumbani na katika sekta nyinginezo.







